Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli amesaini kitabu cha Maombolezo katika Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es salaam


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli amesaini kitabu cha Maombolezo katika Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es salaam kufuatia vifo vya watu zaidi 130 vilivyotokea November 15, 2015 kutokana na mashambulizi ya ugaidi mjini Paris, Ufaransa.

Pamoja na kutia saini kitabu cha maombolezo, Mheshimiwa Dr. Magufuli ametoa salamu za pole kwa Rais wa Ufaransa Mheshimiwa Francois Hollande na kumuombea uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu

Dokta Magufuli ambaye amepokelewa na Balozi wa Ufaransa hapa Nchini Bibi Malika Berak amesema Tanzania imeguswa na vifo hivyo na inaungana na Ufaransa katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Aidha Rais Magufuli amewaombea majeruhi wote wa tukio hilo wapone haraka ili waweze kuungan a na familia zao na kuendelea na shughuli zao za kila siku

Katika hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli amewasili Mjini Dodoma jioni hii kwa shughuli mbalimbali za kikazi.

Mheshimiwa Magufuli amesafiri kwa gari kutoka Dar es salaam hadi Dodoma na taarifa ya shughuli atakazozifanya mtaarifiwa baadaye.

 

Imetolewa na;

Gerson Msigwa

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

IKULU

November 17, 2015