Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 30 Januari, 2016 amewaapisha Balozi, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania na Makatibu Tawala wawili


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 30 Januari, 2016 amewaapisha Balozi, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania na Makatibu Tawala wawili, Ikulu Jijini Dar es salaam.

Walioapishwa ni:

  1. Balozi Mahadhi Juma Maalim, ambaye anakuwa Balozi mpya wa Tanzania nchini Kuwait.

 

  1. Luteni Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, ambaye anakuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) akijaza nafasi iliyoachwa wazi na Luteni Jenerali Samuel Albert Ndomba, ambaye amestaafu. Kabla ya Uteuzi huu Luteni Jenerali Mabeyo alikuwa Mkuu wa Usalama na Utambuzi wa Jeshi la wananchi Tanzania.

 

  1. Kamishna Paul Moses Chagonja, ambaye anakuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, akijaza nafasi iliyoachwa wazi Madeni Kipande ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

 

  1. Kamishna Clodwig Mathew Mtweve, ambaye anakuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, akijaza nafasi iliyoachwa wazi na Faisal Issa ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

 

Akizungumza baada ya kuapishwa, Balozi Mpya wa Tanzania nchini Kuwait Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim, ameahidi kuiwakilisha vyema Tanzania nchini Kuwait hususani katika uchumi ili Tanzania iweze kunufaika na ushirikiano uliopo baina ya mataifa haya mawili.

 

Nae Mnadhimu Mkuu wa Jeshi wa wananchi Tanzania Luteni Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, ameahidi kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na Mtangulizi wake Luteni Jenerali Mstaafu Samuel Albert Ndomba ya kuhakikisha anamshauri vizuri Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na hivyo kuliwezesha Jeshi hilo kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

 

Kwa upande wao, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Kamishna Clodwig Mathew Mtweve na Katibu wa Mkoa wa Katavi Kamishna Paul Moses Chagonja, wameahidi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa katika kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye mikoa waliyopangiwa, ikiwemo kusimamia nidhamu kwa watumishi wa umma.

 

Gerson Msigwa,

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Dar es salaam

30 Januari, 2016