Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Dkt. Edward Hoseah


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Dkt. Edward Hoseah kutokana na kutorishwa na namna taasisi hiyo ilivyokua ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa hususani kwenye upotevu wa mapato ya serikali katika bandari ya Dar es salaam.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kufuatia kutenguliwa kwa uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bwana VALENTINO MLOWOLA kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.

Balozi Sefue amebainisha kuwa, Rais Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa utendaji kazi wa TAKUKURU chini ya Dkt. Edward Hoseah hauwezi kuendana na kazi anayoitaka.

"Eneo mojawapo la upotevu mkubwa wa mapato ya serikali ni Bandarini na Katika Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Hivyo Mheshimiwa Rais amesikitishwa na kitendo cha taarifa za kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika eneo hilo kwa muda mrefu lakini kasi ya TAKUKURU kuchukua hatua haiendani na kasi anayoitaka" amesisitiza Balozi Sefue

Katika hatua nyingine Balozi Sefue amesema, Rais Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU ambao walisafiri nje ya nchi licha  ya Rais Magufuli kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma.

Watumishi hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha safari kutoka kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.

Balozi Sefue amewataka watumishi wengine wa umma kutii agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na kuonya kuwa atakayekiuka atachukuliwa hatua kali.

 

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

16 Desemba, 2015