Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN APOKEA UJUMBE MAALUM KUTOKA KWA RAIS WA RWANDA PAUL KAGAME, IKULU CHAMWINO LEO TAREHE 03 JUNI, 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 03 Juni, 2021 amepokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame uliowasilishwa na Mjumbe Maalum na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda, Mhe. Dkt. Vincent Biruta.

Katika ujumbe huo, Mhe. Rais Kagame ametuma salamu za pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kupokea kijiti cha Urais na amemhakikishia kuwa Rwanda ipo tayari kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania.

 

Katika mazungumzo hayo Mhe. Rais Kagame amesema hali ya Rwanda ni shwari na ipo tayari kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania hususan katika utekelezaji wa miradi ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo na ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge railway) ya kuunganisha Jiji la Kigali (Rwanda) na Isaka (Tanzania) ambayo itasaidia usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Rwanda.