Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

RAIS SAMIA: NDUGAI ATAENZIWA KWA MAGEUZI NA MAENDELEO


RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongoza waombolezaji kuaga mwili wa Mbunge wa Kongwa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Job Yustino Ndugai, leo katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.

Rais Dkt. Samia amesema msiba huu ni pigo kwa taifa, akimtaja marehemu kama kiongozi shupavu, mzalendo na mkomavu kisiasa ambaye mchango wake utaendelea kuishi katika mioyo ya Watanzania.

“Tumempoteza nguzo muhimu, aliyeaminiwa ndani na nje ya nchi, aliyejituma bila kuchoka katika kulinda maslahi ya Taifa letu,” alisema Rais Dkt. Samia.

Kadhalika, ameeleza kuwa Hayati Ndugai aliongoza mageuzi makubwa, ikiwemo kuingiza Bunge katika mfumo wa kidijitali kupitia ‘Bunge Mtandao’, mfumo uliowezesha shughuli za Bunge kufanyika kisasa zaidi, kwa ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji,” alisema.

Aidha, Rais Dkt. Samia amemkumbuka Ndugai kwa kusimamia ukamilishaji kwa Jengo la Utawala Annex lenye kumbi tisa za kisasa za mikutano, pamoja na kuanzisha Kamati Maalum Nne za ushauri kwa Serikali kuhusu rasilimali muhimu za taifa kama almasi, tanzanite, gesi na uvuvi wa bahari kuu.

“Mapendekezo ya kamati hizi yalisaidia kuimarisha usimamizi wa rasilimali na kuongeza mchango wake kwenye pato la taifa,” aliongeza Rais Dkt. Samia.

Rais Dkt. Samia pia amekumbusha nafasi ya Ndugai katika mchakato wa kutangazwa Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi, akirejea agizo lake la kihistoria la mwaka 2017 lililowezesha kutungwa kwa sheria hiyo.

Akizungumzia mchango wake kwa jamii, Rais Dkt. Samia amemuelezea Ndugai kama kiongozi: “aliyependa maendeleo ya vijana, hasa wasichana, na alihakikisha wanafika mbali kielimu,” na kuongeza kuwa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bunge iliyopo Kikombo, Dodoma ulikamilika asilimia kubwa kwa jitihada zake.

Kwa upande wa jimbo la Kongwa, Rais Dkt. Samia amesema maendeleo yaliyopatikana ni ushahidi wa jitihada za kiongozi huyo, akitaja ongezeko la shule za msingi kutoka 50 mwaka 2000 hadi 131, sekondari kutoka 3 hadi 45, vituo vya afya kutoka 3 hadi 10, na vijiji vyote kufikiwa na umeme.

Hayati Job Yustino Ndugai alifariki dunia tarehe 06 Agosti, 2025 jijini Dodoma, akiacha kumbukumbu ya utumishi wa miaka 25 kama Mbunge wa Kongwa na mchango mkubwa katika uongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.