Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

RAIS SAMIA ASHIRIKI MKUTANO WA 36 WA UMOJA WA AFRIKA (AU) JIJINI ADDIS ABABA NCHINI ETHIOPIA TAREHE 17-19 FEBRUARI, 2023


Tarehe 16 Februari, 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).

 

 

Kabla ya kuanza kwa mkutano huo, tarehe 17 Februari, 2023 Rais Samia alishiriki Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika Jengo la Usalama na Amani la Julius Nyerere lililopo katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) Addis Ababa nchini Ethiopia.

 

Mkutano huo ulifuatiwa na Mkutano wa Baraza la Amani na Usalama (PSC) la Umoja wa Afrika (AU) pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kujadili hali ya Usalama katika eneo la Mashariki ya Jamhuri ya  Kidemokrasia ya Kongo (DRC) siku hiyo hiyo chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa tarehe 17 Februari, 2023.

 

Tarehe 18 Februari, 2023 Rais Samia alitoa hotuba ya kujitambulisha katika Mkutano wa 36 wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika katika Ukumbi wa Nelson Mandela kwenye Makao Makuu ya Umoja huo.

 

Akizungumza wakati akitoa hotuba hiyo, Rais. Samia alisema alikuwa na jukumua la kulileta taifa pamoja na kujipanga upya kuendeleza masuala yalioachwa na mtangulizi wake aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Rais John Pombe Magufuli.

 

Aidha, Rais Samia alisema katika kipindi cha miaka miwili amekutana na wadau wa siasa wa ndani ya nchi na makundi mbalimbali ili kuliweka taifa pamoja.

 

Vile vile, Rais Samia aliwahakikishia kuwa Tanzania itaendeleza misingi ile ile ya Sera ya mambo ya nje iliyowekwa na waasisi wa taifa letu.

 

Wakati huo huo, Rais Samia aliwashukuru na kuwapongeza Wakuu wa Nchi na Serikali kwa kupitisha Azimio la kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya AU ambao umemuwezesha leo kuhutubia Mkutano huo kwa lugha hiyo.

 

Kwa upande mwingine, Rais Samia aliwaalika Wakuu wa nchi na Serikali katika Mkutano wa Kilele cha Jukwaa la Kijani (Alliance for Green Revolution High Level Forum-AGRF) utakaofanyika kuanzia tarehe 4 - 8 Septemba, 2023.

 

Rais Samia alieleza kuwa Mkutano huo utajadili masuala ya Mifumo ya Chakula barani Afrika (African Food Systems) kwa kushirikiana na Wakulima, Wafanyabiashara na Wadau mbalimbali kutoka nchi za Afrika na nje ya Bara la Afrika.

 

Mbali na kushiriki Mkutano huo, Rais Samia alikutana na kuzungumza na Viongozi wa Taasisi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Dkt. Abiy Ahmed, Rais wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema, Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Kundi la Mashirika ya Ndege ya Ethiopia Girma Wake, pamoja na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Bi. Victoria Kwakwa.