Habari
RAIS SAMIA AFANYA ZIARA YA KIKAZI MKOANI KAGERA KUANZIA TAREHE 08 – 10 JUNI, 2022
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya ziara ya siku tatu mkoani Kagera kuanzia tarehe 08 -10 Juni, 2022.
Akiwa njiani kuelekea mkoani Kagera akitokea uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita Mhe. Rais Samia alisimama njiani kusalimia wananchi katika maeneo ya Bwanga wilaya ya chato mkoa wa Geita, Biharamulo mkoani Kagera, Muleba Mkoani Kagera na Izibo Mkoani Kagera.
Tarehe 09 Juni, 2022, Mhe. Rais Samia alitembelea kiwanda cha Sukari cha Kagera Sugar kilichopo Missenyi mkoani humo ambapo aliwataka wawekezaji katika viwanda vya sukari nchini kuchangia kikamilifu kufanikisha malengo ya kujitosheleza.
Rais Samia amesema Serikali imeazimia kufanya mageuzi ya kilimo cha kisasa ambayo yanapaswa kwenda sambamba na mahitaji ya viwanda vya ndani ili kuifanya nchi iweze kuwa mzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo Afrika.
Katika kutekeleza mageuzi hayo, Rais Samia amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha alizeti na michikichi mkoani humo.
Mh. Rais Samia amesema lengo la kuanzisha kilimo cha mazao hayo ni kuzalisha mafuta ya kujitosheleza ndani ya nchi, kuwawezesha vijana kujiajiri na kuinua uchumi wa Mkoa huo.
Aidha, Mhe. Rais Samia amewahakikishia wawekezaji kuwa Serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya uwekezaji kwa kurekebisha Sera, Sheria na Kanuni zitakazochochea uwekezaji endelevu.
Rais Samia pia alizindua Mradi wa maji wa Kyaka- Bunazi wilayani Missenyi na kisha kuhutubia wananchi wa mkoa wa Kagera katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Tarehe 10 Juni, 2022 Mhe. Rais Samia alifungua Msikiti wa JAMI’UL ISTIQAMA Bukoba mjini, Mkoani Kagera na kurejea jijini Dodoma kuendelea na shughuli za kiserikali.