Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

RAIS SAMIA AFANYA ZIARA YA KIKAZI MIKOA YA GEITA NA KIGOMA KUANZIA TAREHE 15 – 18 OKTOBA, 2022


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya ziara ya kikazi ya kuanzia tarehe 15-18 Oktoba, 2022 katika Mikoa ya Geita na Kigoma.

 

Akiwa Mkoani geita tarehe 15 Oktoba, 2022, Rais Samia alizuru kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na kukagua Jengo la Makumbusho la Hayati John Magufuli.

 

Mhe. Rais Samia pia alitembelea na kukagua Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato mkoani Geita na kisha kuzungumza na wananchi wa Buseresere  na Katoro mkoani humo.

 

Vile vile Mhe. Rais Samia alizindua kituo cha kupokea, kupooza na kusambaza umeme cha Mpomvu, kufungua Kiwanda cha kusafisha dhahabu kilichopo mkoani Geita (GGR) Chenye uwezo wa kuhifadhi dhahabu tani 50 na baadae kuzungumza na wananchi wa mkoani Geita katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa CCM wa Kalangalala, Geita mjini.

 

Tarehe 16 Oktoba, 2022 Mhe. Rais Samia alihitimisha ziara yake kwa kuzungumza na Wananchi wa Runzewe mkoani Geita na kuzindua miradi sita ya umeme ikiwemo njia ya kusafirisha umeme wa msongo kv 220 Nyakanazi – Geita, Nyakanazi – Rusumo na njia  kubwa za kusafirisha umeme kwenda mkoa wa Kigoma na kuzungumza na wananachi wa Nyakanazi wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.

 

Mhe. Rais Samia alianza ziara ya kikazi mkoani Kigoma kwa kuzindua Skimu ya maji ya Kakonko- Kizigizigu  iliyopo mlima Kanyamfisi  wilaya ya kakonko wilayani Kigoma.

 

Aidha, Mhe, Rais Samia alifungua hospitali ya Wilaya ya Kakonko na kisha kufungua barabara ya Kabingo – Nyakanazi yenye urefu wa kilomita 50 ambayo imekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.

 

Hali kadhalika, Mhe. Rais Samia alihutubia wananchi wa Kibondo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kibondo.

 

Tarehe 17 Oktoba, 2022 alihutubia wananchi katika uwanja wa Mvugwe, wilayani Kasulu, aliweka Jiwe la Msingi mradi wa ujenzi wa barabara ya kabingo- Kibondo – Kasulu- Manyovu  yenye urefu wa kilomita 260.6.

 

Vile vile Mhe. Rais Samia alizindua umeme wa gridi ya taifa na kuzima umeme wa jenereta kutoka megawatt 14 hadi megawatt 20 wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

 

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema kuzinduliwa kwa gridi hiyo kutawezesha mkoa wa Kigoma utapata umeme wa moja kwa moja na wa uhakika ambao utavutia wawekezaji mkoani humo na hivyo kukuza uchumi.

 

Mhe. Rais Samia pia alizindua majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga wilayani Kasulu ambayo yamejengwa na Serikali chini ya Mradi wa Kuboresha Mafunzo ya Ualimu Tanzania (TESP).

 

Sambamba na hilo, Mhe. Rais Samia pia alizindua na kuweka Jiwe la Msingi ujenzi wa barabara ya Manyovu - Kasulu - Kibondo - Kabingo/Kakonko, kufungua barabara ya Kidahwe – Kasulu pamoja na kufungua Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe kabla ya kuzungumza na wananchi Manyovu/ Mnanila.

 

Tarehe 18 Oktoba, 2022, Mhe. Rais Samia aliweka Jiwe la Msingi upanuzi wa bandari Ndogo ya Kibirizi katika Makao Makuu ya Bandari ya Ziwa Tanganyika  na kisha kuweka Jiwe la Msingi Jengo la kutolea Huduma za Wagonjwa wa Dharura (EMD) na Wagonjwa wa Uangalizi Maalum (ICU) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Maweni mkoani Kigoma.

 

Mhe. Rais Samia alihitimisha ziara yake kwa kuhutubia wananachi wa Mkoa wa Kigoma katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa michezo wa Lake Tanganyika na kisha kurejea jijini Dar es Salaam kuendelea na majukumu yake ya kila siku.