Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

RAIS SAMIA AFANYA ZIARA YA KIKAZI KATIKA MIKOA YA MBEYA, NJOMBE NA IRINGA KUANZIA TAREHE 05 - 13 AGOSTI, 2022


Kuanzia tarehe 05 Agosti hadi tarehe 13 Agosti, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya kikazi katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Njombe na Iringa).

 

Tarehe 05 Agosti, 2022 Rais Samia alizindua Mradi wa Maji wa Mbalizi (Shongo - Igale) mkoani humo ambao uligharimu kiasi cha shilingi BILIONI 3.345 utahudumia vijiji nane na wananchi zaidi ya elfu 80.

 

Mradi huo unakamilisha Ilani ya CCM ya kufikia asilimia 95 kwa wananchi wa Mbalizi ikiwa ni ahadi iliyotolewa katika Kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

 

Rais Samia pia alisimama na kuzungumza na Wananchi wa mbalizi ambapo ilielezwa kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kutafuta mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya njia nne kutoka Uyole mpaka uwanja wa ndege kupitia hospitali ya Mbalizi yenye urefu wa kilomita 5.

 

Barabara hii ikikamilika itaunganisha Mbalizi na Songwe na nchi Jirani ya Malawi na kukuza uchumi wa Mbeya inatarajiwa kuanza kwa kuwa ipo katika bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2022/2023.

 

Serikali imeruhusu Wakulima wa Mbalizi kuuza pareto ya unga na Serikali imeshatoa vibali viwili kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya pareto mkoani humo.

 

Serikali imeongeza bajeti ya TARURA katika Halmashauri ya Mbalizi kutoka shilingi bilioni 1.4 hadi bilioni 2.4.

 

Serikali pia imejenga vituo vya afya vya Ifupa, Swaya na mwaka huu kituo cha afya kitajengwa Mbalizi.

 

Katika siku hiyo ya kwanza ya ziara yake Mhe. Rais Samia aliweka jiwe la msingi katika jengo la mama na mtoto hospitali ya Meta linalogharimu shilingi bilioni 11.

 

Kukamilika kwa jengo la kutolea huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali hiyo kutaongeza idadi ya wakina mama wajawazito wanaofika kujifungua katika Hospitali hiyo kutoka mama wajawazito 150 kwa sasa hadi kufikia 300 kwa wakati mmoja na kuhudumia kina mama wa mkoa huo na kutoka mikoa mingine ya Nyanda za juu Kusini.

 

Vile vile Rais Samia ameweka Jiwe la Msingi katika jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ililogharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.

 

Tarehe 06 Agosti, 2022 Rais Samia alianza ziara katika Wilaya ya Chunya, Mhe. Rais Samia alikagua na kuzindua mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya Makongolosi kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 39 uliogharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 67.

 

Rais Samia pia alizindua mradi wa maji wa Makongolosi uliogharimu shilingi bilioni 2.8.

 

Akiwa njiani kuelekea Chunya Rais Samia aliwasalimia wananchi wa Chalangwa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya ambapo katika Wilaya ya Chunya Serikali inatekeleza mirasi zaidi ya sita kwa gharama shilingi bilioni 15.

 

Katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya ujenzi wa barabara Wilayani Chunya.

 

Serikali ilijenga hospitali ya Wilaya ya Chunya ambayo hapo awali ilikuwa kituo cha afya.  

 

Serikali imeweka mazingira mazuri ya wachimbaji madini ya dhahabu katika Wilaya ya Chunya ambapo imesaidia Wilaya hiyo kuwa ya pili kwa uzalishaji wa madini ya dhahabu nchini na Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuwapelekea umeme wachimbaji wenye Plant ili kuweza kuzalisha zaidi.

 

Tarehe 07 Agosti, 2022 Rais Samia alizindua mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya Chuo cha Ualimu cha Mpuguso uliogharimu shilingi bilioni 39.8. Ukarabati huo wa vyuo vya walimu (Upgrading of Teacher’s College) ni mabweni, mabwalo pamoja na maabara.

 

Rais Samia aliweka jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha pamoja cha forodha katika eneo la Kasumulu mpakani mwa Tanzania na Malawi Wilayani Kyela mkoani Mbeya.

 

Ujenzi huo unatekelezwa na China Geo-Engineering Corporation (CGC) na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Engineering Consultant Group (ECG) kutoka Misri.

 

Kukamilika kwa kituo hicho kitasaidia kukuza uchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kwa kuwa kitawezesha wananchi kufanya biashara kwa urahisi na kujiletea maendeleo.

 

Mradi huo pia unahusisha jengo la abiria lenye sehemu za kukagua mazao na bidhaa nyingine. Pia kuna sehemu za usalama kwa ajili ya kupima afya za abiria na endapo itabainika kuna mgonjwa, ipo sehemu ya Karantini ya kumhifadhi mgonjwa huyo kwa muda.

 

Rais Samia pia alizindua barabara ya Kikusya – Ipinda – Matema Wilayani Kyela kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 39.1

 

Serikali imejenga vituo vya afya vinne kwa zaidi ya shilingi bilioni 2 na shilingi trilioni mbili zinatumika kujenga Hospitali ya Wilaya ya Kyela.

 

Tarehe 08 Agosti, 2022 Rais Samia alishiriki katika maadhimisho ya kilele cha siku ya Wakulima nchini (Nanenane)`.

 

Rais Samia amewataka wakulima kutumia maeneo hayo yatakayotengwa kuzalisha kibiashara ili kupata chakula cha kutosha na kuuza kwa nchi jirani.

 

Rais Samia pia alimuelekeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi kushirikiana na Chuo cha Kilimo (SUA) ili kuwezesha vijana wanaohitimu chuoni hapo kuweza kujiajiri katika sekta hiyo.

 

Rais Samia alihitimisha ziara yake mkoani Mbeya na kuelekea Mkoani Iringa ambapo akiwa njiani kuelekea Iringa, Rais Samia alisimama na kuwasalimia wananchi wa Chimala Wilayani Mbarali.

 

Tarehe 09 Agosti, 2022 Rais Samia alianza ziara mkoani Njombe na kuweka jiwe la msingi katika Chuo cha VETA cha Wilaya ya Mbarali kilichojengwa katika Kijiji cha Mwaganga wilayani humo mkoani Mbeya.

 

Rais Samia amesema Chuo cha VETA Mbarali kitafungua fursa kwa wanambarali kupata mafunzo ya ufundi Stadi na kwenda kutoa huduma kwa wananchi.

 

Wilaya ya Mbarali ni miongoni mwa Wilaya 25 wanufaika wa mradi wa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya Wilaya ulioanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2019/2020.

 

Ujenzi wa vyuo hivi ulianza kupitia mradi wa ambapo Serikali ilitenga Shilingi za Kitanzania Bilioni 40, sawa na Shilingi Bilioni 1.6 kwa kila Chuo kwa ajili ya kuanza kazi za ujenzi.

 

Kupitia Mpango wa maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 Serikali ilitenga tena jumla ya Shilingi bilioni 28.76 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyuo hivyo pamoja na gharama za kutengeneza samani.

 

Chuo hicho kinatarajiwa kuhudumia wakazi wote wa Wilaya hii na maeneo ya jirani na mradi wa ujenzi wa Chuo hicho una jumla ya majengo kumi na saba (17) ambayo ni Jengo la utawala, karakana 4, Jengo la madarasa, Mabweni mawili Bwalo la chakula, Majengo tatu ya Maliwato, Nyumba ya Mkuu wa Chuo, Nyumba ya familia mbili za watumishi, Jengo la mitambo ya umeme, Jengo la stoo na Jengo la ofisi ya walinzi.

 

Ujenzi wa Chuo hicho utakapokamilika kinatarajiwa kuanza na fani tisa za muda mrefu na mfupi na kudahili jumla ya wanafunzi 240.  

 

Mhe. Rais Samia alianza ziara yake katika Mkoa wa Njombe ambapo alikagua na kutembelea Ujenzi wa Mradi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.

 

Rais Samia alipokea taarifa ya Mradi na kuweka jiwe la msingi katika Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Njombe – Moronga – Makete km 107.4 eneo la Iwawa Mabehewani – Makete

 

Tarehe 10 Agosti, 2022 Rais Samia alikagua na kuzindua Soko Kuu la Njombe mjini ambalo lina uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara wasiopungua 630 na limegharimu thamani ya shilingi Bilioni 10.2

 

Kutembelea na kukagua kinu cha kufua umeme, kiwanda cha Miwatina kiwanda cha Plywood katika eneo la kiwanda cha TANWAT.

 

Kiwanda Cha TANWATT kinajihusisha na uzalishaji wa nguzo za umeme, Dawa ya kutibu Ngozi (Tanin), plywood, mbao na umeme Megawatt 2 ambapo 0.7 megawatt wanatumia wenyewe na Megawatt 1.3 wanawauzia Tanesco.

 

Rais Samia alizungumza na wananchi wa Njombe katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Saba saba  mjini Njombe.

 

 

Tarehe 11 Agosti, 2022 Rais Samia alianza ziara mkoani Njombe ambapo aliweka Jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Sawala - Mkonge - Iyegera - Lulanda yenye urefu wa Kilometa 40.7 inayojengwa kwa kiwango cha Lami katika wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa.

Ujenzi wa barabara  hiyo unatekelezwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini Tanzania (TARURA) chini ya mkandarasi Hematec Inverstment Ltd na G'S Contructors Co Ltd.

Barabara hiyo ni mojawapo ya barabara zilizochaguliwa chini ya Programu ya Agriconnect awamu ya kwanza kwa Wilaya za Kilolo (km 18.3) na Mufindi (km 30.3) kwa Mkoa wa Iringa zenye jumla ya km 48.6 na Mbeya vijijini (km 26.8) na Rungwe (km 12.2) kwa Mkoa wa Mbeya km 38.4.

Kilometa 30.3 kati ya km 40.7 zimeshawekwa tabaka la lami nyepesi na usanifu wa sehemu iliyobaki ya km 10.4 unaendelea na utakamilika mwezi Oktoba 2022. Utekelezaji wa Sehemu iliyobaki utafanyika mwaka wa fedha 2023/24.

Jumla ya Shilingi bilioni 8.76 zimeshalipwa ambapo sehemu ya kwanza zimelipwa Shilingi bilioni 4.1 na sehemu ya pili zimelipwa Shilingi bilioni 4.66.

Mradi huu wa kimkakati una lengo kusaidia wakulima vijijini katika kuongeza na kuimarisha mnyororo wa thamani ya mazao ya wakulima wa Mufindi hasa mazao ya mbogamboga, kahawa, chai na mazao mengine yanayohitaji kusafirishwa kutoka maeneo ya uzalishaji hadi kufika viwandani na katika masoko pasipo kupoteza ubora wake.

 

Tarehe 12 Agosti, 2022 Mhe. Rais Samia akiweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Iringa.

 

Mradi huo utakapokamilika utarahisisha shughuli za utalii hasa kwa wageni wanaokwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na vivutio vingine.

Pia, uwanja huo utaongeza kasi ya ukuaji wa biashara katika mikoa ya Nyanda za Juu kusini hususan kutokana na uzalishaji wa mazao mengi kama parachichi, chai na mazao ya miti.

Rais Samia alifanya alizungumza na wananchi wa Iringa katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa CCM Samora, Iringa Mjini.

 

Tarehe 13 Agosti, 2022 Rais Samia alihitimisha ziara yake mkoani Iringa na kurejea Jijini Dodoma.

 

Akiwa njiani kuelekea jijini Dodoma, Rais Samia alisimama na kuwasalimia wananchi wa Ismani Tarafani mkoani Iringa na wananchi wa Mpunguzi Mkoani Dodoma.