Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Rais Kikwete aondoka nchini kwa ziara rasmi ya Kiserikali ya siku nne katika Jamhuri ya India


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete yuko njiani kwenda India ambako atafanya ziara rasmi ya Kiserikali ya siku nne katika Jamhuri ya India kwa mwaliko wa Rais wa India, Mheshimiwa Pranab Mukherjee. Ziara hiyo, inaanza rasmi jioni ya Jumatano, Juni 17, 2015.

Wakati wa ziara yake, Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete, mbali na kukutana na Rais Mukherjee kwa mazungumzo rasmi ya Kiserikali, atakutana kwa mazungumzo na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mohammad Hamid Ansari na Waziri Mkuu Narendra Damordadas Modi, ambaye aliingia madarakani rasmi Mei 26, mwaka jana, 2014 akiwa Waziri wa 15 wa Jamhuri ya India baada ya chama chake cha Bharatiya Janata Party (BJP)  kushinda uchaguzi mkuu.

Ziara hii itakuwa ya pili kwa Rais Kikwete kutembelea India katika miaka 10 ya uongozi wake. Mwaka 2008, Rais Kikwete, akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), alitembelea India ambako alikuwa Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi za Afrika na India (India-Africa Forum) uliofanyika mjini New Delhi, mji mkuu wa India pamoja na Waziri Mkuu wa India wakati huo, Mheshimiwa Manmohan Singh.

Wakati wa ziara yake, Rais Kikwete atatembelea miji ya New Delhi na Jaypur (Pink City of India) na miongoni mwa shughuli zake ni kukutana na Watanzania ambao wanaishi India, kukutana na wafanyabiashara wakubwa wa India wenye kutaka kuwekeza Tanzania na na kufungua Mkutano wa Kwanza wa Wafanyabiashara wa Tanzania na India (1st Indian-Tanzania Business Forum).

Mbali na wafanyabiashara, kiasi cha wanafunzi 2,500 wa Kitanzania wanasoma katika vyuo vikuu vya India kwa ufadhili wa Serikali za Tanzania na India. Hawa ni mbali na maelfu ya wanafunzi ambao wanajisomesha wenyewe katika vyuo vikuu vya nchi hiyo.

Rais pia atakutana kwa mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la India, Air India, kwa nia ya kulishawishi shirika hilo kuanzisha tena safari za ndege kati ya nchi hizo mbili, atakutana na Mtendaji Mkuu wa Benki ya ICICI, benki kubwa binafsi kuliko zote katika India, ambayo inataka kuingia ubia na Benki ya Posta Tanzania, atakutana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Infrastructure Leasing and Financial Services ambayo inataka kujenga barabara ya kisasa kabisa kati ya Dar es Salaam na Chalinze na miradi mikubwa ya maji.

Aidha, Rais Kikwete atakutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Kundi la Makampuni ya Hospitali za Apollo ambayo inataka kujenga hospitali kubwa na ya kisasa Kigamboni, Dar Es Salaam.

Rais Kikwete pia atatembelea kiwanda cha kutengeneza matrekta cha Fiat New Holland ambacho kimekuwa kinashirikiana kwa karibu na Kampuni ya Biashara ya Jeshi la Kujenga Taifa ya SUMA JKT na baadaye kutembelea Shirika la Taifa la Viwanda Vidogo la India.

Rais Kikwete ataungana na Waziri Mkuu Modi kushuhudia utiaji saini wa mikataba minne kati ya Tanzania na India katika maeneo ya utalii, maji na miundombinu.

Ziara ya Rais Kikwete katika India inatoa nafasi ya kuimarisha uhusiano wa kihistoria, wa karibu na wa kirafiki ambao una historia ndefu na ya karne nyingi  na ambao uliimarishwa zaidi na uhusiano rasmi ambao ulianzishwa miaka 54 iliyopita. Kimsingi uhusiano huo umejengwa katika misingi ya biashara na mahusiano ya watu kwa watu.

India ndiyo nchi inayofanya biashara kubwa zaidi duniani na Tanzania. Mwaka 2013-14, biashara hiyo ilikadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni nne. Mbali na uhusiano wa biashara, Watanzania wengi wamekuwa wanasaka huduma za afya na elimu katika India. Inakadiriwa kuwa tokea mwaka 1999 kiasi cha Watanzania 4,100 wamepata huduma za afya katika hospitali za Apollo pekee.

Inakadiriwa kuwa kuna wananchi kati ya 50,000 na 60,000 wenye asili ya India (PIO’s) ambao wanaishi na kufanya kazi katika Tanzania.

Imetolewa na;

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu – Dar es Salaam.

17 Juni, 2015