Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Rais kikwete aanza ziara rasmi Uingereza


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini London, Uingereza, kwa ziara rasmi ya siku tatu ya kidola, moja ya ziara nadra sana kufanywa na viongozi wa nchi za nje nchini Uingereza.

Rais Kikwete na ujumbe wake aliondoka nchini usiku wa jana, Jumamosi, Machi 29, 2014, kuelekea London kwa ziara hiyo ya siku tatu ambako atakuwa Mgeni Rasmi wa Serikali ya Uingereza.

Katika ziara hiyo, Rais Kikwete ambaye ameambatana na Mama Salma Kikwete pia anafuatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Bernard Membe, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mheshimiwa Hussein Mwinyi, Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Harrison George Mwakyembe, Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Sospeter Muhongo, Waziri wa Fedha Mheshimiwa Saada Makuya na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Nassoro Mazrui.

Rais pia anafutana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali (mst) J. Simbakalia na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Tekolojia Mheshimiwa January Makamba.

Baada ya ziara ya Uingereza, Rais Kikwete atakwenda Brussels, Ubelgiji kuhudhuria Mkutano wa Wanne wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Afrika – EU-Africa Summit - uliopangwa kufanyika kwa siku mbili – Jumatano na Alhamisi, wiki ijayo kwenye Makao Makuu wa EU mjini Brussels.

Mkutano huo ambao mada yake kuu itakuwa ni Umuhimu wa Kuwekeza katika Watu, Ustawi na Amani utahudhuriwa na wakuu wa nchi wanachama wa EU na wale wa Afrika akiwamo Rais Kikwete.

Mikutano ya wakuu wan chi za EU na Afrika imefanyika mara tatu mpaka sasa kuanzia na ule wa kwanza wa mwaka 2000 mjini Cairo, Misri ukifuatiwa na ule wa Lisbon, Ureno mwaka 2007 na Tripoli, Libya  mwaka 2010.

Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kuhudhuria mkutano huo tokea ashike mamlaka ya kuongoza Tanzania mwishoni mwa 2005.

 

Rais Kikwete pia ameombwa kuhuduria mikutano mingine kadhaa ambayo itafanyika wakati wa Mkutano huo mkubwa.

           

Mwisho.

Imetolewa na;

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu –Dar es Salaam.

30 Machi,2014