Habari
RAIS DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE ATOA HATI YA URAIA KWA WALIOKUWA WAKIMBIZI WA BURUNDI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jioni ya jana, Jumanne, Oktoba 14, 2014, alitoa Hati za Uraia wa Tanzania kwa wakimbizi 162 ambao walikuwa wakimbizi kutoka Burundi na ambao wameishi nchini kwa miaka 42, tokea Mwaka 1972.
Rais Kikwete ametoa Hati hizo katika shughuli fupi iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora ikiwa sehemu ya shughuli za Rais Kikwete katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo. Kwa niaba ya wenzao, Rais Kikwete ametoa Hati hizo kwa wakimbizi hao 19 wa zamani kwa niaba ya wenzao.
Shughuli hiyo ya utoaji Hati za Uraia ilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Mathias Chikawe, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi nchini na mabalozi wa Uingereza, Canada, Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, Ireland,Ubelgiji na mwakilishi wa Ubalozi wa Japan pamoja na Askofu Mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Tabora.
Shughuli ya leo inakamilisha mchakato mbao ulianzishwa na Rais Kikwete Mwaka 2007 wakati alipoamua kuwapa wakimbizi hao wa Burundi uraia wa Tanzania baada ya kuwa wameishi nchini kama wakimbizi tokea walipoingia kwa mara ya kwanza Mwaka 1972 kufuatia machafuko katika Burundi. Wameishi katika kambi za ukimbizi katika Wilaya ya Kaliua, Mkoa wa Tabora.
Akizungumza katika shughuli hiyo, Mwakilishi wa UNHCR katika Tanzania, Bi. Joyce Mends-Cole amesema kuwa Tanzania imekuwa nchi ya kwanza katika historia ya dunia kwa kutoa uraia kwa watu wengi kiasi hicho na kwa wakati mmoja.
Naye Balozi wa Ireland nchini Mheshimiwa Fionnula Gilsenan, akizungumza kwa niaba ya mabalozi wenzake ameisifu sana Tanzania na kumpongeza Rais Kikwete kwa uamuzi wa kutoa Uraia na Hati za Uraia kuwa ”kitendo kikubwa na kitendo kizuri sana.”
“Mheshimiwa Rais umefanya kitu kikubwa mno. Hili ni jambo kubwa na wewe mwenyewe umeshuhudia furaha ya watu hawa. Umesikia nyimbo zao za shukurani kwako na kwa Serikali.”
Akizungumza na raia hao wapya wa Tanzania, Rais Kikwete amesema kuwa matarajio yake na yale ya Watanzania ni kuwaomba raia wapya ni kuwaona wakitimiza ahadi yao kwa nchi yao kwa kuwa raia wapya.
“Shughuli ya leo ni kutimiza tu mchakato kwa sababu hili la uraia wenu tulilimaliza siku nyingi. Matarajio yangu na yale ya Watanzania wenzenu ni nyie kutimiza ahadi ya kiapo chenu cha kuwa raia wema wa nchi yenu. Heshimuni kiapo chenu.”