Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

RAIS APEWA TUZO YA UTAWALA BORA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametaja misingi mikuu mitano ambayo utekelekezaji wake unathibitisha kushamiri kwa utawala bora nchini.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa pamoja na kwamba utawala bora unaendelea kushamiri nchini, bado taasisi za usimamizi wa masuala ya utawala bora zina nafasi ya kuboresha kazi yao na kupanua kwa kiasi kikubwa zaidi utawala bora.

Rais Kikwete aliyasema hayo usiku wa jana, Jumatatu, Juni 23, 2014, wakati alipozungumza baada ya kuwa ametunukiwa Tuzo ya Kutambua Mchango Wake wa Kuimarisha Utawala Bora nchini ambayo imetolewa na taasisi nane za usimamizi nchini.

Taasisi hizo ni Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCB), Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA), Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali (ACCGen-D), Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (IAG-D) na Sekretarieti ya Tume ya Maadili.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa Tuzo hiyo kutolewa nchini na ilikabidhiwa kwa Rais Kikwete wakati wa chakula cha usiku kilichoandaliwa kwa ajili ya wajumbe wa Mkutano wa Mwaka wa Wakaguzi wa Hesabu za Serikali kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) mjini Dar Es salaam.

Mkutano huo wa mwaka pia unahudhuriwa na wajumbe waalikwa kutoka nchi za Ujerumani, Afrika Kusini, Uganda, Sweden, Sierra Leone, Nigeria, Niger, Ghana, Kenya, Zambia, Rwanda, Burundi na Ethiopia.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa Tuzo hiyo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bwana Ludovick Utoh, Rais Kikwete alisema kuwa Tanzania ina utawala bora kwa sababu inadumisha misingi yote mikuu ya utawala bora.

Aliitaja misingi hiyo kuwa ni kushamiri wa demokrasia, uhuru wa kutoa maoni na wa vyombo vya habari, haki ya kila Mtanzania kuishi, utawala wa sheria, kutoingiliana kwa mihimili mitatu ya Serikali.

Rais Kikwete ambaye amesema kuwa amepokea Tuzo hiyo kwa niaba ya viongozi wenzake katika Serikali – Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Katibu Mkuu Kiongozi, Makatibu Wakuu na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama – amesema kuwa utawala bora ni jambo muhimu na halina mbadala wake.

“Tanzania tumeruhusu uhuru mkubwa kwa wananchi wetu kushiriki katika shughuli zao. Serikali yetu haitishi watu wake. Hatufanyi hivyo. Ziko nchi zinaishi kwa kutisha raia wake na nyie mnazijua, “ alisema Rais Kikwete.