Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

RAIS - AMPOKEA MWANA WA MFALME WA JAPAN


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete asubuhi ya leo, Alhamisi, Julai 3, 2014, amemkaribisha Ikulu, Dar Es Salaam, Mwana wa Mfalme wa Japan, Prince Akishino pamoja na mkewe Princess Akishono.

Mwana Mfamle huyo ambaye anatembelea Tanzania, amewasili Ikulu kiasi cha saa nne asubuhi na kufanya mazungumzo ya zaidi ya nusu saa na Mheshimiwa Rais Kikwete.

Katika mazungumzo yao, Rais Kikwete amesema kuwa Japan ni mshirika mkubwa na muhimu sana wa maendeleo ya Tanzania. “Tunathamini sana mchango wenu katika maendeleo ya Tanzania na tunaendelea kuwashukuru sana. Ukizunguka nchini mwetu utaona kwa macho yako miradi mingi na mikubwa ambayo imejengwa ama inajengwa kwa msaada wa Japan.”

Rais kikwete ameongeza: “Pamoja na ushirikiano huu. Bado tunaamini kuwa Japan inaweza kusaidia zaidi Tanzania hasa kwa kushawishi makampuni yake kuwekeza katika sekta binafsi. Ukipita mitaa ya Dar es Salaam, magari tisa kati ya 10 ni ya Kijapan. Ukiingia katika maduka ya vyombo vya elektroniki  - televisheni, kompyuta, camera, karibu kila kitu kinatoka Japan. Hali hii inathibitisha kuwa bidhaa vya Japan zina soko kubwa na zinaweza kuzalishwa hata hapa nchini na makampuni binafsi.”

Rais Kikwete pia ameitaka Japan kuangalia jinsi gani inavyoweza kusaidia ongezeko la watalii kutoka Japan kuja kutembelea Tanzania kwa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka huko hadi Tanzania na nchi nyingine za Afrika.

“Wataalii wengi kutoka Japan wanashindwa kuja Afrika kwa sababu hakuna shirika hata moja la ndege la Japan ambalo lina safari za kuja Afrika, hata Afrika Kusini hakuna. Hii ndiyo maana hatuoni watalii wengine kutoka nchi za kusini mashariki mwa Bara la Asia kutembelea vivutio vyetu vya utalii,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Kama kuna jambo halionekani sasa katika uhusiano wa Tanzania na Japan ni uwekezaji katika sekta binafsi. Hili ndilo jambo tunaloliomba.”

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

IKULU

DAR ES SALAAM

3 Julai, 2014