Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

RAIS - AKUTANA NA WAANGALIZI WA EAC


Waangalizi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki wameshangazwa na amani na utulivu uliokuwepo wakati wa kupiga kura.

Kiongozi wa Timu ya waangalizi wa Uchaguzi Mkuu kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Ndugu Moody Awori, ambaye pia ni Makamu wa Rais Mstaafu wa Kenya amemueleza Rais Jakaya Mrisho Kikwete alipofika Ikulu leo mchana.

“Sisi kutoka Kenya tulishangaa, unakwenda kwenye kituo watu wako kimya, tunakupongeza pamoja na Chama Cha Mapinduzi”  Ndugu Awori amemueleza Rais na kuongeza kuwa, “Tunatarajia kuwa uongozi mpya unaoingia madarakani utafuata nyayo zako” amesema.

Ndugu Awori amemueleza Rais kuwa katika shughuli zao za uangalizi, walitembelea vituo zaidi ya 12 kwa siku jijini Dar es Salaam na kote hali ilikuwa shwari na kueleza kuwa wamejifunza kitu kikubwa sana katika uchaguzi huu.

Watanzania kwa jadi yao ni watu wa amani na utulivu lakini pia kabla ya uchaguzi, Rais Kikwete aliweka wazi kuwa Serikali yake ina wajibu wa kulinda watu na mali zao na kuhakikisha watu wote wanashiriki katika kupata haki yao ya kupiga kura kwa amani, uhuru na utulivu bila kubughudhiwa na hilo ndiyo jambo kubwa na la msingi kwa Serikali yake.

Mapema leo asubuhi Rais Kikwete amehudhuria hafla ya kukabidhiwa vyeti kwa washindi wa uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu  Dkt. John Pombe Magufuli, Rais Mteule na Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Mteule .

Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Vyama na Serikali pamoja na Viongozi wa Waangalizi wa Uchaguzi hapa nchini, Viongozi wa dini na watu mbalimbali.

Baadaye Rais Kikwete aliongoza mapokezi ya Rais Mteule katika Ofisi ndogo za CCM Lumumba ambako wanachama, mashabiki na wapenzi wa CCM walifika kumpokea na kumsalimia mgombea wao ambaye ameibuka mshindi wa Uchaguzi  Mkuu wa mwaka 2015.

 

……………………..MWISHO……………………..

Imetolewa na:

Premi Kibanga,

Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

30 Oktoba, 2015