Habari
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Juni 23, 2014, amekutana na kufanya mazungumzo na tajiri mkubwa zaidi barani Afrika, Mfanyabiashara Aliko Dangote wa Nigeria.
Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Bwana Dangote amemweleza Rais Kikwete kuhusu maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha saruji ambacho kinajengwa na kampuni ya Bwana Dangote mjini Mtwara.
Bwana Dangote amemweleza Rais Kikwete kuwa kiwanda hicho cha Mtwara kitakuwa kikubwa zaidi kuliko kiwanda chochote cha saruji katika ukanda wa Afrika mashariki, kati na kusini isipokuwa kile kinachojengwa Afrika Kusini.
Rais Kikwete amekuwa anaweka msukumo wa kipekee katika ujenzi wa kiwanda hicho kwa nia ya kuongeza uwekezaji nchini na pia kuinua kiwango cha saruji nchini.
Katika jitihada zake hizo, Rais Kikwete mwezi uliopita alifanya ziara katika kiwanda kikubwa zaidi kuliko vyote vya saruji katika Afrika kinachomilikiwa na Bwana Dangote nchini Nigeria.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR ES SALAAM
23 Juni, 2014