Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Taarifa kwa vyombo vya Habari


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 30 Machi, 2019 amewatunuku Kamisheni Maafisa wapya 146 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kundi la 65/18 katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Sherehe za kuwatunuku Kamisheni Maafisa hao zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda.

Akitoa maelezo ya sherehe hizo Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) Brig. Jen Stephen Justice Mnkande amesema Maafisa hao wapya walianza mafunzo tarehe 12 Machi, 2018 wakiwa 236 ambapo 94 kati yao wameshindwa kufuzu kutokana na sababu mbalimbali, na kwamba 146 waliofuzu wamefundishwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na kukubalika kimataifa.

 Brig. Jen Mnkande ameongeza kuwa Maafisa wapya waliotunukiwa Kamisheni katika cheo cha Luteni Usu wana viwango mbalimbali vya elimu ambapo 3 wana Shahada ya Uzamili, 116 wana Shahada ya Kwanza, 3 wana Shahada ya Juu na 23 ni Madaktari wa binadamu.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuendelea kuiamini, kutoa kipaumbele na kuitumia JWTZ katika majukumu mbalimbali ya kuwahudumia wananchi na ameahidi kuwa Jeshi hilo litaendelea kutimiza wajibu wake kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu ikiwa ni pamoja na majukumu ya kijamii.

Akizungumza na Majenerali, Maafisa, Askari na wageni waalikwa, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Maafisa wapya wa JWTZ kwa kufuzu mafunzo yao na pia ameipongeza JWTZ kwa kutekeleza majukumu yake vizuri, kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.

Mhe. Rais Magufuli ameelezea kuridhishwa kwake na kazi nzuri za kijamii zilizofanywa na JWTZ zikiwemo ujenzi wa ukuta katika eneo la madini ya Tanzanite mkoani Manyara kwa miezi 3, uamshaji wa kivuko cha MV Nyerere kilichopata ajali katika ziwa Victoria uliotumia siku 7, ujenzi wa nyumba 41 katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma kwa miezi 2 na kukusanya korosho za wakulima katika msimu uliopita.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa JWTZ kupitia shirika lake la Nyumbu kutengeneza magari ya zimamoto kama ambavyo shirikia hilo limewahi kufanya katika miaka ya nyuma, ili nchi iondokane na gharama kubwa zinazotumika kuagiza magari ya zima moto kutoka nje ya nchi.

Ameliahidi Jeshi hilo kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha linajiimarisha katika majukumu yake yote na ametoa wito kwa Maafisa wapya kutambua kuwa wapo katika Jeshi linaloheshimika na hivyo wanao wajibu wa kuhakikisha wanaendeleza sifa hiyo njema.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

30 Machi, 2019