Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MKUTANO WA UCHUMI DUNIANI AFRIKA (WORLD ECONOMIC FORUM AFRICA)


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili kwenye mji mkuu wa Nigeria wa Abuja usiku wa jana, Jumanne, Mei 6, 2014 kuhudhuria Kongamano Uchumi Duniani (WEF) kwa Bara la Afrika – World Economic Forum Africa -  linaloanza leo.

Rais Kikwete amewasili kujiunga na marais 13 na wajumbe zaidi ya 1,000 ambao watahudhuria Kongamano hilo la siku tatu ikiwa ni mara ya tatu kwa Kongamano hilo kufanyika nje ya mji wa Cape Town wa Afrika Kusini. Nchi ya kwanza nje ya Afrika Kusini kuandaa Kongamano hili ilikuwa Tanzania, ikifuatiwa na Ethiopia na sasa Nigeria.

Rais Kikwete ambaye amehudhuria karibu kila Kongamano la WEF tokea kuingia madarakani mwaka 2005, amepangiwa kushiriki katika mikutano mitano mikuu hata kama awali wenyewe walikuwa wamemwomba kushiriki katika mikutano 12 ya Kongamano hilo ambalo kaulimbiu yake ni “Kujenga ukuaji unaomshirikisha kila mtu pamoja na kutengeneza nafasi za ajira.”

Baadaye mchana wa leo (Jumatano), Rais Kikwete atashiriki na kuzungumza katika mkutano wa Baraza la Uongozi (Leadeship Council Meeting) ambao umeandaliwa chini ya Visheni Mpya Kilimo ya WEF na unafanyika kwa WEF kushirikiana na Umoja wa Afrika na NEPAD na ambao utahudhuriwa na Wakuu wa nchi na Serikali, Mawaziri wa Maendeleo wa Kundi la Nchi Tajiri zenye viwanda za G8 na viongozi wa AU na NEPAD.

Rais Kikwete pia atashiriki katika mkutano wa Uwekezaji katika Kilimo wa Grow Africa Investment Forum na baadaye jioni atahudhuria hafla ambako Rais wa Nigeria, Mheshimiwa Goodluck Jonathan atawakaribisha wakuu wa nchi na Serikali wanaoshiriki katika Kongamano la WEF-A.

Kesho (Alhamisi), Rais Kikwete atashiriki katika mkutano utakaozungumzia jinsi ya kuboresha miundombinu katika Afrika ambao ni muhimu kwa Tanzania kwa sababu Njia ya Kati ya Tanzania (Central Corridor) imeteuliwa kuendelezwa miongoni mwa njia 51 za Afrika ambazo zilijadiliwa katika Kongamano la WEF la mwanzoni mwa mwaka huu mjini Davos, Uswisi. Rais pia atashiriki katika mikutano mingine miwili.

Mbali na mikutano hiyo, Rais Kikwete amepangiwa kukutana na viongozi maarufu duniani akiwamo Waziri Mkuu wa China Mheshimiwa Li Keqiang, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Mheshimiwa Gordon Brown, Mtawala Mkuu wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID) Dr. Rajiv Shah, Waziri wa Biashara wa Marekani Balozi Michael Froman na Rais wa Sera za Kimataifa, Uhamasishaji na Mipango ya Maendeleo ya nchi mbali mbali ya Taasisi ya Gates Foundation Bwana Mark Suzman.

 

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu.

Dar es Salaam.

7 Mei, 2014