Habari
Mjadala Bunge Maalum la Katiba halininyimi usingizi Rais Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete amesema kuwa hana wasiwasi na hali ya mjadala mkali uliotawala
Bunge Maalum la Katiba kwa sababu ni muhimu kwa mjadala kuhusu Katiba
Mpya ukawa wa kina ili kuweza kupata Katiba bora kwa Watanzania.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Katiba ya Tanzania haitapatikana
kwa mikutano ya kisiasa nje ya Bunge Maalum la Katiba bali ndani ya Bunge hilo
ambako ni dhahiri kuwa mjadala utatawaliwa na nguvu ya hoja na busara.
Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na
Usalama ametoa ufafanuzi huo mchana wa leo, Ijumaa, Juni 20, 2014, wakati
alipotoa Mhadhara (Lecture) kuhusu Usalama wa Taifa (The Security of the
Nation) kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi – National Defence College – kilichoko
Kunduchi, Dar Es salaam.
Wakati wa kipindi cha maswali na majibu, ofisa mmoja wa Jeshi la
Kenya alimwuuliza Rais Kikwete kama alikuwa na wasiwasi kuhusu mjadala
unaoendelea nchini kuhusu Katiba Mpya unaweza kuvuruga usalama wa
Tanzania.
Rais Kikwete amemjibu: “Sina wasiwasi hata kidogo kwa sababu
hatukutarajia kuwa mjadala wa Bunge Maalum la Katiba kuhusu jambo hili kubwa
ungekuwa rahisi. Yalipojitokeza maoni ya Tanzania kupata Katiba Mpya, tuliunda
Tume na tume hiyo ikatoa ripoti yake ambayo ndiyo inajadiliwa katika Bunge
Maalum. Hatukutarajia kuwa mjadala kuhusu ripoti ungekuwa rahisi kwa wajumbe
kutoa majibu ya ndiyo ama hapana.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kinachoendelea ni jambo muhimu na la
lazima...najua wakati mwingine majadiliano yalikuwa makali mno lakini hili ni jambo
zuri. Aina ya mfumo na muundo wa Serikali lilizusha mjadala mkali lakini hayo ni
matokeo ya hali halisi ya masuala yanayojadiliwa.”
“Ni imani yangu kuwa tutafikia mwisho. Mwisho upi, hilo ni suala la Wajumbe
wa Bunge Maalum la Katiba kuamua. Muhimu ni kwamba Katiba Mpya inaweza
kupatikana kutoka Bungeni tu siyo kupitia mikutano ya hadhara nje ya Bunge. Huko
hakuna Katiba huko kuna mikutano ya hadhara na siasa tu. Katiba itapatikana kwa
mijadala na kwa nguvu ya hoja ndani ya Bunge letu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR ES SALAAM
20 Juni, 2014