Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MIAKA 50 YA UHURU MSUMBIJI: SAMIA APONGEZA MAFANIKIO


RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Jamhuri ya Msumbiji kwa mafanikio makubwa ya maendeleo katika kipindi cha miaka 50 tangu ipate uhuru wake, akisema taifa hilo limejenga misingi imara ya ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa raia wake.

Akihutubia tarehe 25 Juni, 2025 katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Msumbiji, jijini Maputo, Rais Dkt. Samia alisema maendeleo ya taifa hilo sio tu ni alama ya ushindi dhidi ya ukoloni, bali pia ni dira ya matumaini kwa mataifa mengine ya Afrika.

“Msumbiji ya leo imejenga mustakabali mpya wa uhuru, heshima na ustawi wa pamoja kwa raia wake,” alisema Rais Dkt. Samia.

Kadhalika, Rais Dkt. Samia alisifu juhudi zilizowekwa na nchi hiyo katika sekta ya elimu, afya, miundombinu na huduma za jamii, akieleza kuwa hatua kama kupunguza vifo vya wajawazito ni ushahidi wa dhamira ya kweli ya kujenga jamii jumuishi.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia alipongeza mchango wa wanawake wa Msumbiji waliojitoa kuwa mstari wa mbele kwenye harakati za mapambano ya uhuru wa nchi yao.

Alitaja mafanikio ya Kikosi cha Wanawake (Feamale Detachment) cha FRELIMO kilichoasisiwa mwaka 1967 kama mfano wa mapinduzi ya kijinsia, na kuwapongeza viongozi wa Msumbiji kwa kuendeleza maono hayo hadi leo.

“Kaulimbiu yenu ya mwaka huu, ‘Miaka 50: Kuwainua Wanawake, Kujenga Usawa wa Kijinsia’ ni ushahidi wa dhamira hiyo endelevu,” alisema Rais Dkt. Samia.

Alihitimisha kwa kusema kuwa mafanikio ya Msumbiji ni kielelezo kuwa uhuru wa kweli una maana zaidi ya kisiasa na unapaswa kugusa maisha ya watu kwa undani.