Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. SAMIA SULUHU HASSAN, ASHIRIKI KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA DEMOKRASIA ILIYOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA DIAMOND JUBILEE JIJINI DAR ES SALAAM TAREHE 15 SEPTEMBA, 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia iliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam tarehe 15 Septemba, 2021.

 

Katika maadhimisho hayo yaliyokuwa na kaulimbiu “Ajenda ya Mwanamke ni Turufu ya Ushindi” Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amewaomba wanawake nchini kushikamana ili kuhakikisha wanamchagua mwanamke kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

 

Mhe. Rais Samia amewaomba wanawake kuhakikisha kuwa mwaka 2025 wanamuweka madarakani Rais mwanamke kwa kuwa kwa sasa Rais aliyepo madarakani amewekwa kwa kudra ya Mungu na matakwa ya Katiba.

 

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongozwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia kama inavyotamkwa wazi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 3 (1).

 

Pia amesema Tanzania inaongoza kwa Uhuru wa vyombo vya Habari kwa kuwa na vyombo vingi vya habari ambavyo kati ya hivyo asilimia 75 vinamilikiwa na watu binafsi.

 

 

Katika maadhimisho hayo, taasisi ya Azaki ya Tanzania Women Cross – Party Platform/ ULINGO ilimkabidhi Mhe. Rais SamiaTuzo kama kiashiria cha ushindi wa mwanamke Mtanzania.