Habari
MHE. SAMIA SULUHU HASSAN AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI MKUU MSTAAFU WA UINGEREZA MHE. TONY BLAIR, IKULU JIJINI DAR ES SALAAM LEO TAREHE 22 JULAI, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 22 Julai, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Mhe. Tony Blair, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mhe.Tony Blair ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Taasisi ya Mabadiliko Ulimwenguni (Tony Blair Institute for Global Change) amemhakikishia Mhe. Rais Samia kuwa taasisi yake inaunga mkono jitahada mbalimbali anazochukua katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.
Tony Blair Institute for Global Change inafanya kazi katika nchi 16 Afrika na imejikita kutekeleza vipaumbele vya Serikali zao ambapo amsema katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu taasisi yake imejikita zaidi katika masuala ya kukabiliana na janga la UVIKO 19.
Mhe. Tony Blair amesema katika kukabiliana na janga la UVIKO 19, taasisi yake inashughulika zaidi na masuala ya upimaji na usambazaji wa chanjo ambapo amesema taasisi yake inaweza kusaidia Tanzania kuwafikia wazalishaji wa chanjo hizo.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia ameeleza kuwa kwa sasa Serikali inaendelea na uboreshaji wa mazingira bora ya uwekezaji kwa sekta binafsi ili kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) wa Tanzania.
Aidha, Mhe. Rais Samia ameikaribisha taasisi ya Tony Blair kuja nchini kufanya kazi na taasisi za Tanzania kusaidia utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali.