Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA RAIS WA CHAMA CHA WANASHERIA TANGANYIKA (TLS) PROFESA EDWARD HOSEAH NA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAJAJI NA MAHAKIMU WANAWAKE TANZANIA (TAWJA) JAJI JOAQUINE DE-MELLO IKULU CHAMWINO JIJINI DODOMA LEO TAREHE 11 AGOSTI, 2021.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 11 Agosti, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

 

Katika mazungumzo hayo, Mwenyekiti wa TAWJA Mhe. Jaji Joaquine De-Mello amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kushika nafasi ya uongozi na kuwa Rais wa kwanza Mwanamke nchini Tanzania.

 

Mhe. Jaji De-Mello amesema Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA), kinafarijika na uongozi wake kutokana na mambo mbalimbali anayofanya ikiwa ni pamoja na kuzingatia usawa wa kijinsia kwa kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi.

 

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amekishukuru Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA) kwa kazi nzuri inayofanya na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kutekeleza majukumu yao na amepokea changamoto zao na kuahidi kuzifanyia kazi.

 

Vilevile, Mhe. Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambapo Rais wa Chama hicho Profesa Edward Hoseah amesema wameomba kukutana na Mhe. Rais ili kujitambulisha na kuelezea  majukumu yao.

 

Profesa Hoseah amesema pamoja na mambo mengine, TLS ina jukumu la kumshauri Rais, Serikali, Bunge na Mahakama katika masuala mbalimbali ya sheria na utawala bora.

Mhe. Rais ameihakikishia TLS ushirikiano wa kufanya nao kazi kwa karibu ili kuweza kutimiza majukumu yake pia amepokea changamoto zao mbalimbali.