Habari
MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AZINDUA MPANGO WA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO 19
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amezindua Mpango wa Serikali wa Kuinua Uchumi na kukabiliana na janga la Korona, UVIKO -19 wenye thamani ya shilingi trilioni 3.62 katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dododma tarehe 10 Oktoba, 2021.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango huo, Mhe. Rais Samia ameitaka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Taasisi nyingine zitakazonufaika na fedha za mkopo wa Shilingi trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani (International Monetaruy Fund-IMF) kuhakikisha zinatumika katika malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, Mhe. Rais ameitaka sekta binafsi kutumia fursa hiyo kwa kuzalisha bidhaa zitakazotumika katika utekelezaji wa miradi hiyo mfano uzalishaji wa saruji, mabati na nondo ili tusiwe na sababu ya kuchelewa kutumia fedha hizo.
Mhe. Rais Samia ameagiza miradi hiyo itekelezwe na wakandarasi wazawa ili fedha hizo ziendelee kubaki na kuzunguka katika uchumi wetu.
Aidha, amewataka Wakandarasi hao wazawa kuwajibika kwa kufanya kazi kwa ubora, umakini na ufanisi.
Katika Mpango huo ambao unatakiwa kutekelezwa ndani ya miezi 9, Mhe. Rais Samia ametaka kutumika kwa utaratibu wa manunuzi wa single source ili kupunguza urasimu katika ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa miradi hiyo.
Aidha, Mhe. Rais Samia amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba kusimamia na kuondoa urasimu wa misamaha ya kodi katika vifaa na bidhaa zitakazotoka nje ya nchi ambazo zitatumika katika Mpango huo.
Vilevile Mhe. Rais Samia amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Mkaguzi wa Hesabu za ndani kufatilia kwa karibu matumizi ya fedha hizo ili malengo na thamani halisi iweze kuonekana.
Mhe. Rais Samia amezitaka Kamati za Bunge kuisimamia kikamilifu miradi hiyo wakati wa kuitembelea. Pia amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini pamoja na timu zao kuhakikisha wanasimamia vizuri fedha hizo ili ziweze kuleta tija katika miradi hiyo.
Katika hafla hiyo, Mhe. Rais Samia pia amezungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miezi sita na kusema kuwa Miradi yote mikubwa ya kimkakati iliyoasisiwa katika Awamu ya Tano ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Ujenzi wa Bwawa la kufua umeme wa Mwalimu Nyerere (Rufiji), madaraja pamoja na barabara, inaendelea vizuri na inatarajiwa kukamilika katika muda uliokusudiwa.