Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AZINDUA MKAKATI WA UELIMISHAJI NA UHAMASISHAJI WA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2022 KATIKA UWANJA WA JAMHURI JIJINI DODOMA TAREHE 14 SEPTEMBA, 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amezindua Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma tarehe 14 Septemba, 2021.

 

Mhe. Rais Samia amesema Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika mwaka 2022 ina lengo la kufahamu idadi ya watu, mahali walipo, jinsia, rika, elimu, ajira, shughuli, makazi yao, mahali yalipo na hali yake.

 

Mhe. Rais Samia amesema taarifa hizo zitasaidia kufahamu wastani wa ongezeko la idadi ya watu katika nchi na pia hali ya uhamiaji kutoka vijijini kwenda mijini na kuwezesha nchi kutambua hatua mbalimbali za kimaendeleo.

 

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema Sensa inasaidia Serikali kufanya maamuzi kuhusu ugawaji wa rasilimali za Taifa na kupeleka huduma mbalimbali za jamii kwa wananchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu kwenye maeneo yao kulingana na idadi ya watu na mahitaji.

 

Mhe. Rais ameelezea kuwa Sensa ya mwaka 2022, itawezesha kutambua idadi ya majengo na mahali yalipo, kufahamu hali ya mahitaji ya makazi nchini na kufahamu na kupanga mitaa kupitia anuani za makazi ambazo zitachochea benki kutoa mikopo na kupunguza viwango vya riba.