Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan azindua Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery Limited mkoani Mwanza tarehe 13 Juni, 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akitembelea kiwanda cha kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery Limited kujionea hatua mbalimbali za upokeaji malighafi, usafishaji pamoja na upatikanaji wa Dhahabu iliyosafishwa. 

 

Akizungumza mara baada ya kuzindua mtambo wa kusafisha dhahabu wa Kampuni ya Mwanza Precious Metals Refinery Limited uliogharimu shilingi bilioni 12.2, amesema mtambo huo utaongeza mapato ya Serikali kupitia mrabaha,tozo za ukaguzi na ushuru wa huduma na kutoa ajira za moja kwa moja 120 na zisizo za moja kwa moja 400.

Amesema mtambo huo utachochea ukuaji wa uchumi kwa kuiwezesha Benki Kuu ya Tanzania kununua dhahabu na hivyo kuwezesha nchi kuwa na amana ya dhahabu kwa kiwango kikubwa.

Mhe. Rais Samia ameongeza kuwa mtambo huo utasaidia kuchochea shughuli za uchimbaji madini kwenye Ukanda wa  Ziwa.

Amesema mtambo huo na mingine miwili iliyopo nchini ni matokeo ya mabadiliko ya sheria iliyofanywa na Serikali katika sekta ya madini ambayo imeongeza mapato ya madini kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 528 mwaka 2020.

Mafanikio mengine yanayopatikana kufuatia mabadiliko ya sheria ya madini nchini ni kuanzishwa kwa masoko 39 na vituo 50 vya kuuzia madini, kutolewa kwa leseni nne za usafishaji madini ya dhahabu katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Geita.