Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AZINDUA CHANJO YA UVIKO 19 TAREHE 30 JULAI, 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amezindua utolewaji wa chanjo ya UVIKO 19 na kuongoza Watanzania kupata chanjo hiyo katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 30 Julai, 2021.

Akizungumza kabla ya kuanza zoezi hilo, Mhe. Rais Samia amewatoa hofu Watanzania kuwa chanjo hiyo ni salama na yeye kama Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama asingejitoa mwenyewe kujipeleka kwenye hatari huku akijua kuwa ana majukumu makubwa yanayomtegemea.

Mhe. Rais Samia amewaomba Watanzania kwa hiyari yao kushiriki katika zoezi hilo la  chanjo  hiyo ya UVIKO 19 ila waendelee kujihadhari na ugonjwa huo.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema amekuwa akipokea jumbe mbalimbali za simu kutoka kwa baadhi ya Watanzania wakimuuliza jinsi ya kupata chanjo hizo ambapo amesema kwa sasa Serikali inaendelea kuratibu upatikanaji wa chanjo za kutosha ili kuwezesha wananchi wengi kupata chanjo hizo.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wananchi kuwapuuza wale wote wanaopotosha kuhusu chanjo hizo za UVIKO 19 na kusisitiza kuwa ni salama kwa afya baada ya  wataalam wetu nchini  kujiridhisha kabla ya kuamua kufanyika kwa zoezi hilo.