Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA RELI YA KISASA STANDARD GAUGE RAILWAY (SGR) KUTOKA MWANZA-ISAKA MKOANI MWANZA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 14 Juni, 2021 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa (SGR ) kipande cha Mwanza – Isaka ikiwa ni siku ya 2 ya ziara yake Mkoani Mwanza.

 

Akihutubia wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Mwanza - Isaka yenye urefu wa kilometa 341 ambao utagharimu kiasi cha shilingi Trilioni 3.06,  amesema mradi huo utaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kusafirisha kwa haraka na kwa kiwango kikubwa cha mizigo na watu tofauti na ilivyo sasa.

Mhe. Rais Samia  ameeleza kuwa mradi huu ni sehemu ya mradi mkubwa wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilomita 1,605 ambao utatengeneza ajira 11,000 hivyo kuwataka wana Mwanza kuchangamkia fursa ya ujenzi wa reli hiyo kwa kuwa wavuvi, wakulima na wafugaji watanufaika na reli hiyo ambayo itakuwa na mabehewwa maalum ya kubebea mazao, nyama na samaki.

Aidha amesema reli hiyo itapunguza muda wa kusafiri kati ya Mwanza hadi Dar es Salaam kutoka saa 17 za sasa kwa usafiri wa mabasi hadi saa 8 mradi utakapokamilika.