Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN ASIMIKWA KUWA MKUU WA MACHIFU TANZANIA TAREHE 08 SEPTEMBA, 2021 MWANZA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesimikwa kuwa Mkuu wa Machifu Tanzania tarehe 08 Septemba, 2021 Mkoani Mwanza wakati akifunga Tamasha la Utamaduni lililoandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania.

Kufuatia umuhimu wa Utamaduni, Mhe. Rais Samia amesema Serikali imejipanga kupanua wigo wa vivutio vya utalii, ukiwemo utalii wa utamaduni ambapo tayari ameanza kuchukua hatua za kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii, biashara na uwekezaji nchini kupitia filamu inayoendelea kurekodiwa na Kipindi maarufu cha Royal Tour

Mhe. Rais Samia amesema pamoja na kuwa Utamaduni hutangaza mila na desturi za nchi lakini pia ni biashara na chanzo kikubwa cha mapato kwasababu ni moja ya vivutio vya utalii.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewaomba Machifu hao nchini kwa kushirikiana na Serikali kudumisha amani na usalama ikiwa ni pamoja na kusuluhisha migogoro kwenye jamii zinazowazunguuka.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amewasihi viongozi hao wa kimila kuwahimiza Watanzania kujilinda na janga la UVIKO 19 ikiwa ni pamoja na kupata chanjo na kuwahamaisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa litakalofanyika mwakani 2022.

Katika Tamasha hilo, Machifu wamemtawaza Mhe. Rais Samia kuwa Chifu Mkuu wa Machifu wote nchini na kumpa jina la Chifu Hangaya likiwa na maana ya Nyota ya asubuhi inayong’aa.