Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN ASHIRIKI TAMASHA LA UTAMADUNI MKOANI KILIMANJARO TAREHE 22 JANUARI, 2022


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni Kilimanjaro lililoandaliwa na uongozi wa Machifu wa mkoa huo tarehe 22 Januari, 2022.

Wakati wa uzinduzi wa Tamasha hilo, Mhe. Rais Samia amewapa pole wananchi wa mkoa Kilimanjaro na mikoa mingine kutokana na ukame ulioikumba mikoa hiyo hususan katika maeneo ya ufugaji uliosababishwa na kuchelewa kunyesha kwa mvua na hivyo kupelekea wananchi kupoteza maelfu ya mifugo yao.

Mhe. Rais Samia amewataka wafugaji kushirikiana na Serikali ili kutumia mafunzo waliyoyapata kutokana na janga la ukame kuona namna bora ya kuanza ufugaji wa kisasa usiotegemea mvua katika kupata malisho.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewashukuru Machifu wa mkoa huo kwa kuitikia wito alioutoa mkoani Mwanza na kuelekeza mikoa yote nchini kufanya matamasha ya utamaduni kwa lengo la kuendeleza mila, desturi na utamaduni wa taifa letu ili zisipotee.

Mhe. Rais Samia amesema Serikali iliunda Wizara mahsusi itakayosimamia moja kwa moja shughuli za sanaa, utamaduni na michezo kwasababu ilitambua umuhimu wa sekta hizi katika kutoa ajira, kukuza uchumi wa nchi na kuitangaza nchi kimataifa.

Vile vile, Mhe. Rais Samia ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuendelea kuratibu, kuvikuza na kuviendeleza vikundi vya burudani za kitamaduni ili vizalishe kazi za mikono za utamaduni kama vile ufinyanzi, ususi, upishi, uchongaji pamoja na kuhamasisha mashindano ya tambo, tenzi, nahau na ushairi kwa kutumia mila na usarifu wa lugha ya Kiswahili.

Mhe. Rais Samia amezitaka Wizara zinazoshughulikia utamaduni na utalii kuandaa mkakati wa pamoja wa kuyabaini matamasha ya kimataifa na kimkoa yatakayoboreshwa na kuendeshwa kimkakati ili yaweze kuwavutia wageni kutoka nje na ndani ya nchi na kuitangaza nchi yetu.

Katika kuendeleza na kuimarisha utamaduni, mila na desturi za kitanzania, Mhe. Rais amesema tayari Serikali imeanzisha kanzi data sahihi inayohusu Machifu, na kwamba Serikali imeanza kuweka taarifa sahihi za Machifu na mchango wao katika kupambana na ukoloni.

Mhe. Rais Samia pia amesema kuwa Serikali inaendelea kuyabaini maeneo ya kichifu na kimila na kuyatunza ili yawe sehemu za vivutio vya nchi yetu pamoja na kuibua, kuimarisha na kuhifadhi majengo na zana za zamani ili zibaki kuwa vielelezo vya utamaduni wetu.

Aidha, Mhe. Rais Samia amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Maliasili na Utalii zinaendelea na majadiliano ya urejeshwaji wa mafuvu ya Machifu yaliyochukuliwa wakati wa ukoloni ili yatumike kuelimisha jamii.