Habari
MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN ASHIRIKI KILELE CHA MAADHIMISHO YA MBIO MAALUM ZA MWENGE WA UHURU, CHATO MKOANI GEITA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia, ameshiriki katika kilele cha maadhimisho ya Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru, Kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Mwalimu Nyerere na Wiki ya Vijana yaliyofanyika katika viwanja vya Magufuli wilayani Chato Mkoani Geita tarehe 14 Oktoba, 2021.
Katika hotuba yake Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuifanyia kazi taarifa ya Mbio za Mwenge wa Uhuru na kuwachukulia hatua stahiki wale wataobainika kuhusika na ubadhirifu katika miradi iliyotajwa kuwa na kasoro.
Amesema haiwezekani kufikia maendeleo kama taifa litaendelea kuwa na vitendo vya rushwa na ufisadi, kwani vitendo hivyo ni chanzo cha ukiukwaji wa haki za wananchi, kuwepo kwa mikataba mibovu na ukiukwaji wa taratibu za ujenzi katika miradi ya maendeleo.
Mhe. Rais Samia ametoa tahadhari kwa miradi inayokwenda kutekelezwa kwenye Mpango wa Maendeleo kwa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 kuwa lisijitokeze suala la ubadhirifu na kuwa atasimama imara kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo na miradi mingine.
Akizungumzia juu ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere, amesema Serikali itaendelea kumuenzi Baba wa Taifa, kutokana na ujasiri alioukuwa nao ukiwemo ushupavu wa kuitumikia nchi yake.
Kuhusu sekta ya afya, Mhe. Rais Samia amesema bado hali haiko vizuri kutokana na kuongezeka kwa maradhi yasio ya kuambukiza yakiwemo ya shinikizo la damu, Kisukari, Kifua Kikuu, Ukimwi, Malaria na janga la UVIKO 19, jambo ambalo ni vyema kwa vijana wa Tanzania kuendelea kuchukua tahadhari ya maradhi hayo.
Mhe. Rais Samia, amewataka wananchi kujikinga na UVIKO 19 kwa kuona umuhimu wa kuchanja kwani Serikali tayari imeshasambaza chanjo na kuwaasa vijana kuacha kutumia dawa za kulevya kutokana na athari zake kwa afya.
Mwenge huo wa Uhuru umetembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi 1, 067 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Trilioni 1.2 kutoka sekta za maji, nishati, afya, kilimo, uvuvi, mifugo na miundombinu.
Alipowasili Wilayani Chato, Mhe. Rais Samia alizuru na kuweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli nyumbani kwao Chato mkoani Geita.
Maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru zimefanyika Wilaya ya Chato Mkoani Geita ili kumuenzi aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.