Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AHUDHURIA SHEREHE ZA KUAPISHWA KWA RAIS WA SABA (7) WA ZAMBIA MHE. HAKAINDE HICHILEMA, JIJINI LUSAKA NCHINI ZAMBIA TAREHE 24 AGOSTI, 2021.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amehudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Saba (7) wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema zilizofanyika katika Uwanja wa Taifa wa Mashujaa (National Heroes Stadium), Jijini Lusaka nchini Zambia tarehe 24 Agosti, 2021.

 

Baada ya Sherehe hizo, Mhe. Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Hichilema ambapo amempongeza kwa ushindi wa nafasi ya Urais pamoja na kuwapongeza wananchi wa Zambia kwa kufanya uchaguzi wa amani na  kumuahidi Rais Hichilema kuendeleza ushirikiano na uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Zambia.

 

Mhe. Rais Samia ameeleza umuhimu wa kukuza biashara baina ya Tanzania na Zambia ili uende sambamba na uhusiano wa kihistoria uliokuwepo kati ya nchi hizo mbili.  Mhe. Rais Samia ameiomba Serikali ya  Zambia kuendelea kutumia Bandari ya Dar es Salaam kupitishia mizigo yake, ombi ambalo lilikubaliwa na kuungwa mkono na Mhe. Hichilema.

 

Kwa upande wake Mhe. Rais Hichilema ametoa salamu za rambirambi kwa Mhe. Rais Samia na Watanzania wote kwa kumpoteza Hayati Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Mhe. Rais Hichilema amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kushiriki katika sherehe za uapisho na kuahidi kufanya kazi na nchi zote jirani na utayari wake wa kushirikiana na nchi hizo katika kudumisha urafiki wa kidugu na kihistoria kwa maendeleo ya wananchi wake. 

 

Aidha, Mhe. Rais Hichilema mesisitiza umuhimu wa kukuza biashara kama njia ya  kujenga uchumi wa nchi yake na kuinua maisha ya wananchi wake. Vilevile alizungumzia umuhimu wa Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano hususani kwenye suala zima la kushughulikia changamoto zinazokwamisha ushirikiano ambapo ameahidi kutoa msukumo wa kisiasa kuhakikisha mikutano hiyo inafanyika mara kwa mara.

 

Halikadhalika, Mhe. Rais Samia amemualika Mhe. Rais Hichilema kufanya ziara  Nchini Tanzania, na Mhe. Rais Hichilema amekubali mwaliko huo.