Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AHUTUBIA KATIKA MKUTANO WA COP 26 GLASGOW, NCHINI SCOTLAND


 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amehutubia mkutano wa Wakuu wa nchi wanaoshiriki mkutano wa 26 kuhusu mabadiliko ya tabianchi tarehe 2 Novemba, 2021 Glasgow nchini Scotland.

Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa mataifa yote kuwa juhudi za pamoja zinahitajika kwa kuwa athari za mabadiliko hayo hazichagui nchi zilizoendelea au zinazoendelea.

Mhe. Rais Samia ameeleza namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoiathiri Tanzania katika ardhi ya uzalishaji mali, ongezeko la kina cha bahari, kuyeyuka kwa barafu katika kilele cha Mlima Kilimanjaro,  namna ambavyo kisiwa cha Zanzibar kinavyoathirika kwa ongezeko la kiwango cha joto ambalo linaathiri ekolojia inayovutia watalii.

Aidha, ameongeza kuwa athari hizo zinatokea licha ya Serikali ya Tanzania kuendelea na azma yake ya kutenga hekta milioni 48 kwa ajili ya utunzaji wa misitu.

Mhe. Rais Samia ameeleza pia kuwa Serikali ya Tanzania inao mkakati maalum wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambao umeainisha hatua kadhaa za kuchukua ikiwemo kupunguza athari za hewa ukaa kwa asilimia kati ya 30 na 35 ifikapo mwaka 2030.

Mhe. Rais Samia amehimiza nchi zilizoendelea kutimiza ahadi zao za kuratibu upatikanaji wa kiasi cha Dola za kimarekani bilioni 100 kwa ajili ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi hususan kwa nchi zinazoendelea kwa kueleza kuwa athari zikitokea zitawakumba wote, nchi zilizoendelea na zinazoendelea.