Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AHUTUBIA BARAZA KUU LA UMOJA WA MATAIFA JIJINI NEW YORK, NCHINI MAREKANI.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amehutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 23 Septemba, 2021 Jijini New York, nchini Marekani.

Katika hotuba yake Rais Samia ameihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa katika uongozi wake, Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na mataifa na wadau wengine duniani kutatua changamoto zinazoukabili ulimwengu hivi sasa.

Kuhusu ugonjwa wa Virusi vya Korona, (UVIKO 19), Mhe. Rais Samia pia ameeleza kuwa ugonjwa huo bado unaendelea kupunguza kasi ya kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) katika muda uliopangwa na kwamba kwenye baadhi ya nyanja, taarifa zinaonesha kuwa kumekuwa na athari zilizorudisha nyuma mafanikio yaliyokwishapatikana.

Aidha, Mhe. Rais Samia amezishukuru Taasisi za Kimataifa ikiwemo Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa jitihada zao za kusaidia nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania zisiathirike zaidi kiuchumi.

Vilevile, ameeleza kuwa tangu kuanza kwa UVIKO 19, Tanzania imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali kukabiliana nao ambapo mwezi Julai, 2021 alizindua rasmi programu ya chanjo nchi nzima na kutoa wito kuwa ili watu wengi katika nchi zinazoendelea waweze kupata chanjo, ni vyema hakimiliki ya kuzalisha chanjo hizo itolewa ili uzalishaji ufanyike kwenye nchi nyingi.

Mhe. Rais Samia ametumia hotuba hiyo pia kueleza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kukuza uchumi licha ya changamoto za ugonjwa huo na kwamba baada ya kushuka kwa ukuaji uchumi kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 5.4 hivi sasa Tanzania inafanya jitihada za kuziinua sekta zilizoathirika zaidi na ugonjwa huo, hususan utalii, na pia kuimarisha mazingira ya kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji nchini pamoja na kuimarisha misingi ya utawala bora.

Halikadhalika, Mhe. Rais Samia ameeleza jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika nyanja za uchumi ikiwa ni pamoja na kuweka sera madhubuti na maboresho ya mfumo wa bajeti ili kupunguza idadi ya wanawake na wasichana wanaoishi katika umasikini.

Mhe. Rais Samia amezungumzia pia athari za mabadiliko ya Tabia Nchi na umuhimu wa kuchukua hatua za kukabiliana na janga hilo na kuyasisitiza mataifa yaliyoendelea kutimiza ahadi zao za kutoa Dola za Kimarekani bilioni 100 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025 kama ilivyokubaliwa katika Azimio la Paris.