Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFUNGUA MKUTANO MAALUM WA UCHAGUZI WA VIONGOZI WA JUMUIYA YA TAWALA ZA MITAA TANZANIA (ALAT)


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amefungua Mkutano Maalum wa Uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) na Mamlaka za Serikali za Mitaa uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 27 Septemba, 2021.

 

Akihutubia wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameitaka Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuimarisha usimamizi na udhibiti wa fedha za Serikali ili ziweze kutumika vizuri na kuleta tija katika miradi ya kimkakati na kuwaletea wananchi maendeleo.

 

Aidha, Mhe. Rais Samia ametaka kuimarishwa kwa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia TEHAMA na kubuni vyanzo vipya vya mapato bila kutumia mabavu katika kukusanya tozo na ushuru.

 

Halikadhalika, Mhe. Rais Samia amewaagiza viongozi wa ALAT kuchukua hatua kwa watendaji wote watakaobainika kufanya ubadhirifu ili tija ionekane katika miradi ya maendeleo na kwenye fedha za mikopo ya asilimia 10 zinazotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

 

Vilevile, Mhe. Rais Samia ameitaka Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha inapoandaa mipango ya maendeleo inazingatia Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao ni wa mwisho katika kutekeleza dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025.

Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa Viongozi wa Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata na vijiji kutenga siku maalum kila wiki kusikiliza na kutatua kero za wananchi, zikiwemo za mirathi na migogoro ya ardhi, ambazo zimekithiri nchini.

 

Pia Mhe. Rais Samia amebainisha kuwa kwa sasa kipaumbele kikubwa katika Serikali ya Awamu ya Sita ni kujenga vituo vya afya kwa Tarafa 250, upatikanaji wa maji safi na salama, ujenzi wa barabara pamoja na madarasa.