Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFUNGUA KONGAMANO LA KWANZA LA KUMBUKIZI YA MAISHA YA ALIYEKUWA RAIS WA AWAMU YA TATU, HAYATI BENJAMIN WILLIAM MKAPA JIJINI DAR ES SALAAM TAREHE 14 JULAI, 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefungua kongamano la kwanza la kumbukizi ya maisha ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa lililofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Julai, 2021

 

Akiwahutubia wananchi waliohudhuria kongamano hilo, Mhe. Rais Samia amesema  mchango mkubwa wa Hayati Rais Mkapa wakati wa uhai wake utabaki kama alama katika historia ya taifa letu kwani Hayati Mzee Mkapa alisimamia mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini pamoja na hatua kubwa alizochukua za kutoa fursa zaidi kwa sekta binafsi na kukaribisha uwekezaji nchini.

Mhe. Rais Samia amemuelezea Hayati Rais Mkapa kuwa ni kiongozi aliyeasisi taasisi nyingi nyeti ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Tume ya Kupambana na UKIMWI (TACAIDS) na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) ambazo zimewezesha mageuzi makubwa katika maendeleo ya nchi yetu.

Amesema kwa upande wa Kimataifa, Hayati Rais Mkapa ameacha alama  katika  diplomasia ya kimataifa. Pia alishiriki kikamilifu katika kufufua  Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ushiriki wake katika kurejesha amani nchini Burundi pia alishiriki katika kugeuza uliokua Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) na kuwa Umoja wa Afrika (AU).