Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFANYA ZIARA YA SIKU TATU MKOANI ARUSHA KUANZIA TAREHE 21-23 NOVEMBA, 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan, amefanya ziara ya siku 3 Mkoani Arusha kuanzia tarehe 21-23 Novemba, 2021.

 

Akiwa mkoani humo, Mhe. Rais Samia amewatunuku Kamisheni Maafisa Wanafunzi 118 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kundi la 02/18 wa Shahada ya Sayansi ya Kijeshi  na kundi la 08/18 Jeshi la Anga, katika sherehe zilizofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Jeshi (TMA) Monduli, mkoani Arusha tarehe 22 Novemba, 2021.

 

Akizungumza na Majenerali, Maafisa, Askari na Wageni waalikwa Mhe. Rais Samia amekipongeza Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) na Chuo cha Uhasibu Arusha kwa ubunifu walionyesha katika kutoa mafunzo hayo kwa Maafisa hao wapya wa JWTZ.

 

Aidha, Mhe. Rais Samia amewapongeza pia Wahitimu wote wa mafunzo hayo ya Shahada ya Sayansi ya Kijeshi kwa kufuzu mafunzo yao.

 

Pamoja na kutunuku Kamisheni, Mhe. Rais Samia ametoa zawadi kwa Maafisa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi na kuwavisha mabawa Maafisa wapya wawili kwa niaba ya wenzao ikiwa ni ishara ya kuhitimu mafunzo yao ya urubani.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amefungua Hoteli ya Gran Meliá yenye hadhi ya Nyota Tano iliyopo Jijini Arusha.

 

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Hoteli hiyo, Mhe. Rais Samia amemshukuru Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Hoteli hiyo Bw. Ali Saeed Albwardy kwa uamuzi wake wa kuwekeza nchini kwa kujenga hoteli hiyo ambayo ni moja ya hoteli zenye hadhi kubwa duniani.

Mhe. Rais amesema uwekezaji huo ni ishara ya kuwepo kwa mazingira bora ya utalii nchini na kuwa uzinduzi wa Hoteli hiyo utaiweka Tanzania katika ramani za Hoteli za Gran Meliá, ambapo duniani zipo 350 katika nchi 40.

Tarehe 23 Novemba, 2021, Mhe. Rais Samia amezindua Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa yaliyofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Mhe. Rais Samia amesema jukumu la usalama barabarani sio la Askari wa barabarani peke yao bali  ni la kila mwananchi  katika jamii na hivyo kumtaka kila mwananchi kuwa makini na kuhakikisha matumizi sahihi ya barabara.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema suala la usalama barabarani lipewe uzito wa kuwa ajenda ya kitaifa katika majukwaa pamoja na kuwahusisha kikamilifu washirika wa maendeleo hasa wale ambao wamepiga hatua kubwa katika maendeleo ya nyanja ya usalama barabarani.

Mhe. Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kuwa na msaada kwa wananchi na sio kero kwao ili kujenga mahusiano mazuri katika jamii hali itakayopelekea kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali kwa wakati.

Ametaja baadhi ya kero zinazofanywa na Askari wa usalama barabarani kuwa ni pamoja na kushikilia leseni za madereva kwa muda mrefu, kulazimisha madereva kulipa faini za papo kwa papo kinyume na ilivyo Sheria ya Usalama Barabarani, hivyo kuwataka wahusika kubalika mara moja.

Aidha, Mhe. Rais Samia ameliagiza Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikianana na vyuo vikuu, vyuo vya ufundi  na chuo cha Usafirishaji (NIT) kuwekeza katika utafiti wa suala la usalama barabarani ili kupata suluhu ya kisayansi na kimfumo ya namna ya kupunguza ajali za barabarani.