Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFANYA ZIARA YA SIKU NNE MKOANI MARA KUANZIA TAREHE 04 – 07 FEBRUARI, 2022


 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliafanya ziara ya Siku 4 mkoani Mara kuanzia tarehe 04 hadi 07 Februari, 2022.

 

Akiwa njiani kuelekea mkaoni Mara Mhe. Rais Samia alizungumza na wananchi katika mji wa Lamadi Mkoani Simiyu ambapo Mhe. Rais Samia amemuagiza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja kufungua kituo cha ulinzi katika eneo hilo ili kulinda wananchi wasipate madhara yatokanayo na wanyama pori wakiwemo tembo na viboko.

 

Mhe. Rais Samia pia aliwasalimia wananchi wa Bunda na Kiabakari Mkoani Mara ambapo tarehe 05 Februari, 2022 alikuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya Miaka 45 ya Chama cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika katika Uwanja wa Karume, Musoma Mkoani Mara.

 

Tarehe 06 Februari, 2022 Mhe. Rais Samia aliweka jiwe la msingi katika Mradi wa Maji wa Mugango – Kiabakari – Butiama utakaogharimu shilingi bilioni 70.5 utakapokamilika katika kijiji cha Mugango kilichopo wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara.

 

Mhe. Rais Samia amesema dhamira ya Serikali ni kumtua mama ndoo kichwani na kusambaza huduma ya maji safi na salama kwa wananchi ambapo tayari asilimia 75 ya fedha za mradi zimeshatolewa na mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2022 au mapema Januari, 2023.

 

Mhe. Rais Samia pia aliwahutubia wananchi wa Kwangwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Kwangwa, Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo eneo hilo.

 

Katika mkutano huo Mhe. Rais Samia alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Ally Salum Hapi kuvunja mkataba na Mkandarasi anaejenga barabara ya Makutano hadi Sanzate Mkoani Mara kwa kushindwa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 50 ambayo imeanza kujengwa tangu mwaka 2013 ambayo itagharimu shilingi bilioni 54.5 itakapokamilika pamoja na barabara ya Musoma - Makoja yenye urefu wa kilomita 5 ambayo ilianza kujengwa mwaka 2020 inayogharimu shilingi bilioni 8.2.

 

Mhe. Rais Samia ameagiza uongozi wa mkoa wa Mara kutafuta wakandarasi wenye uwezo wa kifedha na mitambo katika kutekeleza miradi ya maendeleo mkoani humo.

 

Tarehe 07 Februari, 2022 Mhe. Rais Samia akiwa njiani kuelekea Bunda, Mhe. Rais Samia aliwasalimia wananchi wa eneo la Butiama na kuwaahidi wananchi hao kuwa pamoja na na miradi mbalimbali iliyotekelezwa wilayani humo Serikali itaendelea kuwaletea maendeleo zaidi.

 

Akiwa wilayani Butiama, Mhe. Rais Samia pia alitembelea kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na baadae kuzungumza na wananachi wa Bunda katika mkutano wa hadhara  mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa miundombinu ya kusafisha na kutibu maji utakaogharimu shilingi Bilioni 10.6 utakapokamilika, katika viwanja vya Shule ya Msingi Miembeni, wilayani Bunda Mkoani Mara.

 

Katika mkutano huo, Mhe. Rais Samia amewaagiza Wakaguzi wa ndani wa Halmashauri kufanya kazi kwa ufanisi ili kuzuia mianya ya ufujaji na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo.

 

Mhe. Rais Samia amewataka Wakaguzi hao kufanya ukaguzi wa hesabu za fedha za miradi ya maendeleo mapema na kwa kila hatua badala ya kusubiri ukaguzi kufanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

 

Mhe. Rais Samia pia ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mara kuzuia vitendo vya rushwa kwa  kufuatilia hatua zote za matumizi ya fedha katika miradi pindi fedha za miradi zinapokuwa zimetolewa badala ya kungoja ripoti ya Mkaguzi wa Mahesabu ndipo wafuatilie.

 

Mhe. Rais Samia alihitimisha ziara yake ya siku nne mkoani Mara na kuwashukuru wananchi wa mkoa huo kwa mapokezi makubwa waliyompa muda wote akiwa ziarani mkoani humo na kurejea jijini Dodoma.