Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFANYA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU TATU MKOANI TABORA KUANZIA TAREHE 17-19 MEI, 2022


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Tabora kuanzia tarehe 17 -19 Mei, 2022.

 

Akiwa mkoani humo, Mhe. Rais Samia amezindua barabara ya Nyahua- Chaya yenye urefu wa kilomita 85.4 iliyojengwa kwa ushirikiano na Mfuko wa Maendeleo wa Serikali ya Kuwait (KFAED) kwa gharama ya shilingi bilioni 123.9.

 

 

Katika uzinduzi huo, Rais Samia ametoa wito kwa  Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuendelea kusimamia viwango vya ubora na kasi ya utekelezaji wa miradi kwa kuzingatia masharti ya Mikataba.

 

Aidha, Rais Samia amesema barabara hiyo ina umuhimu kwa kuwa inaunganisha kanda mbalimbali za nchi ikiwemo ukanda wa magharibi, wa kati, kaskazini, kusini, eneo la maziwa makuu pamoja na nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo kupitia Kigoma na Katavi.

 

Tarehe 18 Mei, 2022, Mhe. Rais Samia alifungua barabara ya Tabora- Koga – Mpanda yenye urefu wa Kilomita 342.9 katika wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.

 

Vile vile, Rais Samia ametoa rai kwa wananchi kutokuhujumu miundombinu ya barabara pamoja na kuacha kutoa alama za barabarani kwa manufaa ya watumiaji kwa kuwa miundombinu hii inaigharimu Serikali fedha nyingi.

 

Rais Samia ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Tabora ikiwemo kwenye sekta ya elimu, umeme, mawasiliano ya simu, soko la tumbaku pamoja na miundombinu ya barabara.

 

Awali, Mhe. Rais Samia alisimama na kuzungumza na wananchi wa eneo la Kigwa, Wilaya ya Uyui akiwa njiani kuelekea kijiji cha Tura kwa ajili ya uzinduzi wa Barabara hiyo.

 

Kwa upande mwingine, Rais Samia alizungumza na wananchi wa mkoani humo kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika tarehe 19 Mei, 2022 katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora Mjini.

 

Akiwahutubia wananchi katika hadhara hiyo, rais Samia amesema Serikali imeweka mkazo mkubwa katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji kuanzia mwaka wa fedha ujao kwa kuwa sekta hizo zinawagusa wananchi moja kwa moja.

 

Aidha, Rais Samia amesema kilimo cha maeneo makubwa kitasaidia kuondoa uhaba wa bidhaa mbalimbali kama mafuta ya kula hivyo amemuagiza Waziri wa Kilimo kupunguza bajeti ya matumizi ya manunuzi ya mbolea na kuelekeza fedha hizo kwenye kilimo kikubwa.

 

Rais Samia ametoa wito kwa watafiti wa mbegu za kilimo kufanya utafiti wa mbegu bora za kisasa ili wakulima wapate mbegu zitakazowapa mavuno mazuri.

 

Pia, Rais Samia amewaagiza Wakuu wa Mikoa pamoja na Wilaya kuhifadhi chakula kilichopo ili kitoshe kutumika kabla ya kupata mvua zingine za uhakika kwa kuwa mwaka huu mavuno yamekuwa haba kutokana na ukosefu wa mvua.

 

Hali kadhalika, Rais Samia amesema, ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa mvua ambayo inaathiri kilimo, Serikali inaweka mikakati ya kufanya kilimo cha umwagiliaji ambacho hakitotegemea misimu ya mvua.

 

Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya na Maafisa Tawala nchini kuhakikisha kuwa wanasimamia matumizi ya fedha zinazopelekwa katika Halmashauri zao na kuhakikisha zinafanya kazi zilizokusudiwa katika kutoa huduma za kijamii kwa wananchi.

 

Rais samia alihitimisha ziara hiyo na kurejea Jijini Dodoma kuendelea na majukumu ya kikazi.