Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI UFARANSA NA UBELGIJI KUANZIA TAREHE 09 -19 FEBRUARI, 2022


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Jassan amefanya Ziara ya Kikazi nchini Ufaransa na Ubulgiji kuanzia tarehe 09 -19 Februari, 2022.

Akiwa nchini Ufaransa Mhe. Rais Samia alishuhudia uwekwaji wa saini kati ya Serikali ya Tanzania na Ufaransa katika mikataba sita ya makubaliano kwa nia ya kuendeleza uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Miongoni mwa makubaliano hayo ni mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milioni 178 kwa ajili ya kugharamia mradi wa ujenzi wa barabara wa mabasi yaendayo haraka.

Serikali hizo pia zimesaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milioni 80 ili kuimarisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kufikia malengo ya kutoa mikopo ya muda mfupi na mrefu kwa sekta ya kilimo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ametia saini mikataba mengine ya ushirikiano kwa niaba ya serikali.

Pia serikali za Tanzania na Ufaransa zimesaini Tamko la dhamira ya kushirikiana katika eneo la uchumi wa buluu na usalama wa bahari.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia ameyasihi mataifa yote kuheshimu makubaliano na maazimio waliyotia saini, kama wajibu wa kuchukua hatua madhubuti katika kulinda bahari.

Halikadhalika. Mhe. Rais Samia pia alilihutubia Shirikisho la Biashara la Ufaransa (MEDEF) mjini Paris, Ufaransa, Rais Samia amefafanua kuwa Serikali yake inachukua hatua muhimu kuweka mazingira muafaka ya kukuza sekta binafsi.

Mhe. Rais Samia ameeleza kuwa Serikali imefanya mabadiliko makubwa ya kisheria na kitaasisi kwenye sekta binafsi kuhakikisha kuna wepesi wa kuanzisha na kufanya biashara nchini.

Mhe. Rais Samia, amewakaribisha wafanyabiashara kutoka Ufaransa kuwekeza Tanzania katika sekta za mifugo, kilimo, nishati, madini na maeneo mengine yenye fursa.

Akiwa nchini Ufaransa, Mhe. Rais Samia alikutana na kuzungumza na Rais wa Ufaransa Mhe. Emmanuel Macron katika Ikulu ya Elysee mjini Paris.

Tarehe 14 Februari, Mhe. Rais Samia alihitimisha ziara yake ya kikazi nchini Ufaransa na kuendelea na ziara nyingine nchini Ubelgiji ambapo tarehe 15 Februari, 2022, Mhe. Rais Samia Suluhu amefanya mazungumzo na Mhe. Charles Michel, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya (European Council) wakati wa ziara yake rasmi nchini Ubelgiji.

Mhe. Rais samia amesema Serikali ina mipango ya kuanzisha kiwanda cha kuzalisha chanjo za COVID-19 na maradhi mengine ndani ya nchi na kueleza kuwa bajeti ya serikali ya Tanzania kununua chanjo inakadiriwa itaongezeka kutoka shilingi bilioni 26.1 mwaka 2020 hadi bilioni 216 ifikapo mwaka 2030, ambayo ni sababu muhimu ya kujenga kiwanda hicho.

Akiwa nchini Ubelgiji, tarehe 18 Februari, 2022, Mhe. Rais Samia amekutana na kuzungumza na Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya (EC) ambapo Mhe. Von der Leyen ameipatia Serikali ya Tanzania msaada wa Euro milioni 425 ambayo ni sawa na shilingi trilioni 1.15 kutoka Kamisheni ya Umoja wa Ulaya (EC) kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Fedha zilizotolewa zinatarajiwa kutumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo nchini Tanzania.

Akiwa katika ziara katika nchi za Ufaransa na Ubelgiji, Mhe. Rais Samia pia amezungumza na Watanzania waishio katika nchi hizo.

Mhe. Rais Samia amemaliza ziara yake na kurejea nchini leo tarehe 20 februari, 2022.