Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI GHANA KUANZIA TAREHE 24 MEI, 2022


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alifanya Ziara ya Kikazi ya siku tatu Accra nchini Ghana.

 

Akiwa nchini Ghana, Mhe. Rais Samia alishiriki Mjadala  wa Wakuu wa Nchi uliojadili fursa zilizomo na changamoto zinazozikabili Nchi za Afrika ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa bei ya vyakula na matumizi ya nishati endelevu.

 

Akiwa nchini humo, tarehe 25 mei, 2022, Mhe. Rais Samia alipokea Tuzo tuzo ya Babacar Ndiaye (2022) kwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji.

 

Tuzo hiyo alipokea katika Mkutano wa 57 wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambayo hupewa viongozi wa Afrika walio mstari wa mbele katika kuendeleza miundombinu.

 

Katika hafla hiyo, Rais Samia ametoa wito kwa nchi za Afrika kuungana, kuzijenga na kuziwezesha jumuiya za kiuchumi za kikanda na bara zima kwa ujumla.

 

Mhe. Rais Samia amesema lengo la ujenzi wa miundombinu Tanzania ni kuunganisha nchi, ukanda wa Afrika Mashariki na nchi za SADC ili kufikia agenda ya utangamano wa Afrika kiuchumi na kijamii.

 

Mhe. Rais Samia alitembelea kituo cha Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (The African Continental Free Trade Area), katika Ofisi za (AfCFTA)  Jiji la Accra nchini Ghana na kisha kuzuru na kuweka Shada la Maua kwenye Kaburi la aliyekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Ghana Hayati Dkt. Kwame Nkrumah alipotembelea eneo la Makumbusho (Kwame Nkrumah Memorial Park and Mausoleum) katika Jiji la Accra nchini Ghana.

Mhe. Rais Samia alihitimisha Ziara yake nchini Ghana tarehe 26 mei, 2022 na kurejea nchini Tanzania.