Habari
MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFANYA ZIARA MKOANI KILINJARO NA ARUSHA KUANZIA TAREHE 15-18 OKTOBA, 2021
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amefanya ziara katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha kuanzia tarehe 15 -18 Oktoba, 2021. Akiwa mkoani Kilimanjaro, Mhe. Rais Samia amefungua barabara ya Sanya Juu – Elerai yenye urefu wa kilomita 32.2 iliyogharimu shilingi bilioni 62.666 ikiwa ni sehemu ya barabara ya kutoka Boma ng’ombe – Sanya Juu hadi Kamwanga yenye urefu wa kilomita 98.2.
Mhe. Rais Samia amesema ujenzi wa barabara hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali katika kuwatatulia wananchi kero mbalimbali ambapo ujenzi wa kilomita 44 zilizobaki nazo zitajengwa kama ilivyoahidiwa.
Mhe. Rais Samia pia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi mkoani Kilimanjaro litakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 12.7 litakapokamilika ambapo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 70.
Amesema Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo iweze kuwa na hadhi kamili kama hospitali ya Rufaaa mkoani humo.
Vilevile, Mhe. Rais Samia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja jipya la Rau lenye urefu wa mita 20 kutoka upande wa Rau hadi upande wa Mamboleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi litakalogharimu shilingi milioni 910.72 ambapo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 65.
Mhe. Rais Samia amezungumza na wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro katika Uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi na kuwashukuru wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwa na muamko mkubwa wa kuchanja dhidi ya COVID 19 na kuwataka kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Aidha, Mhe. Rais Samia amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa mkoa huo.
Halikadhalika, Mhe. Rais Samia amehudhuria Maadhimisho ya miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro na kufanya uzinduzi wa mnara wa kumbukumbu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa hospitali ya Rufaa ya KCM Pamoja na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo maalum la kutoa huduma za tiba ya Saratani kwa mionzi litakalogharimu shilingi bilioni 4 litakapokamilika, ujenzi ambao unagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100.
Mhe. Rais Samia amesema inafurahisha kuona uongozi wa hospitali hiyo kuamua kuanzisha vitengo vipya mbalimbali vya utoaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi jambo ambalo litaongeza utalii wa tiba kwa wagonjwa wa ndani na nje.
Amesema Serikali imeendelea kushirikiana na hospitali mbalimbali zinazomilikiwa na Taasisi za Dini zinazotoa huduma za tiba ikiwemo Hospitali ya KCMC ili kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa.
Mhe. Rais Samia aliendelea na ziara yake mkoani Arusha ambapo tarehe 17 Oktoba, 2021 alikagua ujenzi wa mradi wa kuboresha huduma ya maji na usafi wa mazingira unaogharimu shilingi bilioni 520, katika eneo la Chekereni mkoani Arusha.
Mhe. Rais Samia amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Arusha, upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika mkoa wote ambapo ujenzi wa mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 75.
Vilevile, Mhe. Rais Samia amefungua Majengo mapya ya Hospitali ya Jiji la Arusha yaliyojengwa kwa kutumia mapato ya ndani ya Halamashauri ya Jiji hilo pamoja na kutembelea mabanda ya wajasiriamali wadogo wa mkoa huo.
Mhe. Rais Samia amekabidhi hundi zenye jumla ya shilingi Bilioni 1.39 kwa vikundi vya wanawake, walemavu na vijana ikiwa ni mkopo kutoka fedha zinatokana na makato ya asilimia 10 ya Hamashauri ya Jiji la Arusha.
Aidha, tarehe 18 oktoba, 2021 Mhe. Rais Samia alifungua kiwanda cha nyama cha Eliya Food Overseas Ltd kilichopo wilaya ya Longido, Mkoani Arusha chenye thamani ya shilingi bilioni 17 na kuahidi kumaliza changamoto ya maji inayoikabili kiwanda hicho ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.
Mara baada ya kufungua kiwanda hicho, Mhe. Rais Samia alizindua mradi wa maji safi na salama uliogharimu shilingi bilioni 15.8 na kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la Stendi Mpya ya Longido mkoani Arusha mara.
Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Longido mkoani Arusha kuwasimamia watumishi wa Wilaya hiyo ili wawe na maadili na nidhamu na kuwachukulia hatua pale watumishi hao wanaopokosea.
Amesema ni lazima viongozi wa Wilaya hiyo kusimamia uwajibikaji katika Halmashauri hiyo kwa kulinda makusanyo ya fedha pamoja na kusimamia nidhamu katika maeneo yao.