Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFANYA MKUTANO NA WANAWAKE JIJINI DODOMA


Rais wa jamhuri ya Muungano Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan leo tarehe 8 Juni, 2021 amefanya mkutano na Wanawake jijini Dadoma katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center. Akiwahutubia wanawake hao, rais samia amewataka wanawake kote nchini kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi ambazo zinazowasaidia katika kusukuma mbele maendeleo yao na ya Taifa kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayo dhamira ya dhati ya kuwaunga mkono.

Mhe. Rais Samia amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu, hadi mwaka jana Tanzania ilikuwa na wanawake zaidi ya Milioni 29.4 ambao ni asilimia 51.04 ya watu wote, hivyo wanawake ni jeshi kubwa ambalo linategemewa katika uchumi na ustawi wa jamii na hawapaswi kubaki nyuma, badala yake watumie fursa mbalimbali zilizopo kufanya mageuzi yatakayolisaidia Taifa kusonga mbele. Mhe. Rais Samia amefafanua kuwa Serikali itaendelea kujenga miundombinu na kuimarisha huduma zitakazowawezesha wanawake kufanya shughuli zao kwa manufaa na tija ikiwemo kujenga miundombinu ya usafiri, elimu, afya, maji na kuwaunganisha na taasisi zinazotoa ujuzi na fedha za kuendeshea biashara.



Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa wanawake wote nchini, kukaa na kutafakari maeneo ambayo wanafanya vizuri na maeneo ambayo hawafanyi vizuri ili kuchukua hatua za kurekebisha dosari na amewata Mawaziri wenye dhamana za afya, elimu na Serikali za Mitaa kushughulikia changamoto za Wanawake ili kurahisisha shughuli zao.

Amewahakikishia Watanzania wote kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuhakikisha inatekeleza ipasavyo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 ikiwemo kuhakikisha usambazaji wa maji Mijini unafikia asilimia 95 na Vijijini asilimia 85, kujenga miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwemo ujenzi wa reli na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato Mkoani Dodoma.