Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE.RAIS - MALENGO YA MILENIA


Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Jumuiya ya Kimataifa  kuhakikisha kuwa malengo ya milenia yanatekelezwa kwa  ukamilifu hata baada ya kuisha muda uliowekwa wa kuyatimiza,  kabla ya kuweka malengo mengine duniani.

Rais Kikwete ametoa ushauri huo  tarehe 28 Mei,2014 mwanzoni mwa  mkutano wa kimataifa unaohusu Afya ya Mama  na Mtoto jijini Toronto Canada, ambapo alikuwa akijibu maswali kuhusu matokeo ya malengo ya milenia kuelekea mwisho wa muda wa kuyatekeleza mwakani 2015.

"Tukamilishe pale ambapo hatujamaliza na kuimarisha yale  yote tuliyoyafanikisha au kuyafikia " Rais amesema na kuwataka Mataifa kuhakikisha kuwa, malengo manane (8) ya milenia waliyojiwekea, yanatekelezwa,kwa ukamilifu kwani ni malengo mazuri na muhimu kwa jamii zetu.

Rais amesema "baada ya kuyaimarisha na kuyatimiza haya malengo manane tunaweza kupanga na kutafuta mengine na pia tuhakikishe kuwa haya ya sasa hayasahauliki wala kutelekezwa ili tusije kurudi nyumba katika jitihada zetu”.

Malengo ya Milenia Kama yalivyoainishwa na Umoja wa Mataifa ambayo nchi zinazoendelea zinatakiwa kuwa zimeyafikia ifikapo mwaka kesho wa 2015 ni pamoja na kuondoa umaskini uliokithiri na njaa,  Elimu ya Msingi kwa  wote, Usawa wa kijinsia na fursa sawa kwa wanawake, kupunguza vifo vya watoto wachanga na upatikanaji wa huduma bora za uzazi.

Mengine ni kupanga na ukimwi, Malaria na magonjwa mengine,kulinda mazingira na kujenga mshikamano wa kimaendeleo duniani.

Mapema tarehe 28 Mei,2014, Rais alikutana  na  wafanyabiashara na wawekezaji wa makampuni mbalimbali ya Canada, ambayo baadhi tayari yana vitega uchumi nchini Tanzani.

Rais amewaeleza wawekezaji fursa ambazo wanaweza kupata iwapo watawekeza Tanzania ikiwemo katika sekta mbalimbali za kiuchumi.


Tarehe 29 Mei,2014  mkutano huu unatarajiwa kuendelea na kuzungumzia njia mbalimbali ambazo Mataifa yanatakiwa kufanya kwa pamoja katika jitihada zao za kuimarisha Afya ya Mama na Mtoto.