Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA ALIYEMALIZA MUDA WAKE HAPA NCHINI WANG KE, IKULU MKOANI DODOMA LEO TAREHE 04 JUNI, 2021.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 04 Juni, 2021 ameagana na aliyekuwa Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke ambaye amemaliza kipindi chake.

Katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma, Mhe. Rais Samia amemshukuru Mhe. Wang Ke kwa jitihada zake za kuendeleza na kukuza uhusiano wa Tanzania na China ambao umewezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na China hapa nchini kama ujenzi wa baadhi ya majengo ya taasisi mbalimbali ikiwemo maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jengo la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lililopo Jijini Dar es Salaam pamoja na kutoa  msaada wa shilingi Bilioni 35 ambazo zimeelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Halikadhalika, Mhe. Rais Samia pia amemshukuru kwa ufadhili wa China katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa huduma za kijamii pamoja na ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji ambao pamoja na kukuza pato la nchi umesaidia Watanzania wengi kupata ajira.

 

Kwa upande wake Mhe. Wang Ke amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa ushirikiano mkubwa alioupata kutoka kwa Serikalini ya Tanzania kwa  kipindi chote alichokuwepo nchini kutekeleza majukumu yake ya kibalozi. Aidha, Balozi Wang Ke amempongeza Rais Samia kwa kupokea kijiti cha Urais kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Mhe. Balozi Wang Ke amewasilisha salamu za Rais wa China Mhe. Xi Jinping ambaye ameeleza kuwa ana imani kubwa kuwa Mhe. Rais Samia atafanya mazuri na makubwa kwa Tanzania kutokana na dhamira yake ya kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na Hayati Dkt. Magufuli hususani uendelezaji wa miradi ya kimkakati, kuchukua hatua madhubuti za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuchukua hatua za kisayansi za kukabiliana na janga la ugonjwa wa Korona (Covid-19).