Habari
Marekani imeipatia Tanzania vitabu vingine milioni 2.5 vya masomo ya sayansi kwa sekondari
Marekani imeipatia Tanzania vitabu vingine milioni 2.5 vya masomo ya sayansi kwa sekondari katika mwendelezo wa nchi hiyo kuisaidia Tanzania kukabiliana na uhaba wa vitabu na walimu wa masomo ya sayansi, Balozi mpya wa Marekani katika Tanzania Mheshimiwa Mark Chilress amesema.
Balozi Childress amezieleza habari hizo njema kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati walipokutana kwa mara ya kwanza tokea balozi huyo alipowasili nchini na kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais kikwete.
Wakati Rais Kikwete akimweleza hali ya utendaji wa sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii nchini na hasa jitihada za Serikali kukabiliana na changamoto za elimu, Balozi Childress amemweleza Rais Kikwete kuwa uchapishaji wa vitabu hivyo umeanza kufuatia uidhinishwaji wa fedha za kuifanya kazi hiyo mwezi uliopita.
“Mheshimiwa Rais ninayo furaha kukujulisha kuwa kazi hiyo imeidhinishwa ifanywe tokea mwezi Mei na kuwa vitabu vitawasili nchini mwanzoni mwa mwaka ujao,” Balozi Childress amemwambia Rais Kikwete ambaye ameshukuru kwa msaada huo mkubwa ambao ni mwendelezo wa misaada ya Marekani katika nyanja ya elimu.
Vitabu hivyo vya sayansi vinakadiriwa kuwa na thamani ya dola za Marekani milioni tisa na vitasafirishwa na kuwasili nchini Januari mwakani kabla ya kufunguliwa kwa shule kwa mwaka mpya wa masomo.
Kama ambavyo imekuwa kwa misaada ya vitabu kutoka Marekani, miswada ya vitabu hivyo vipya imeandaliwa na kuandikwa na wataalam wa taasisi ya Tanzania Institute of Education na kuhakikiwa na wataalam wa masomo hayo ya sayansi – fizikia, kemia na biolojia kabla ya kupelekwa Marekani kwa uchapishaji.
Tanzania ilianza kupata vitabu vya sayansi kwa mara ya kwanza tokea Rais Kikwete alipomwomba Rais wa 43 wa Marekani, Mheshimiwa George W. Bush kuisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto kubwa za ufundishaji masomo ya sayansi mwaka 2008. Vitabu hivyo ambavyo idadi yake ilikuwa milioni tatu viliwasili nchini mwaka 2010 na kugawiwa katika shule mbali mbali za sekondari.
Rais Barack Obama ameendeleza sera ya kutoa msaada wa vitabu vya sayansi kwa Tanzania na inakadiriwa kuwa vitabu vya sasa vitamaliza mahitaji yote ya vitabu vya masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa sekondari nchini kwa angalau miaka miwili ijayo.
Tanzania ina kiasi cha wanafunzi milioni 1.8 katika shule za sekondari nchini kwa sasa na kati ya wanafunzi hao theluthi moja wanachukua masomo ya sayansi.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Kampuni ya Ujenzi wa Reli ya Tanzania Railway Construction Corporation ya China, Bwana Zhang Zongyan pamoja na Mwenyekiti wa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation Bwana Lui Zhimng.