Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MADINI YA URANI YAJA NA FURSA KIBAO KWA TAIFA


RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema mradi wa majaribio wa uchenjuaji wa madini ya urani utazalisha manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Taifa na wananchi, ukiwemo uwekezaji wa kigeni wa Dola za Marekani Bilioni 1.2 na ajira kwa Watanzania.

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa mradi huo wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma unaoendeshwa na kampuni ya Mantra Tanzania Limited kutoka nchini Urusi.

Amesema tathmini ya mradi inaonesha kuwa utadumu kwa miaka 20, ambapo katika kipindi husika ajira zipatazo 3,500 zinatarajiwa kupatikana wakati wa ujenzi wa miundombinu, sambamba na ajira za kudumu 750 na ajira 4,500 kutokana na shughuli nyingine kwenye eneo la mradi.

“Kipaumbele cha ajira kiwe kwa Watanzania na hususan wananchi waliopo katika vijiji na maeneo ya karibu na mradi huu, kwa ajira zisizohitaji ujuzi mkubwa,” amesisitiza Rais Samia.

Serikali inatarajia kupata mapato makubwa ikiwemo mrabaha wa Dola milioni 373, kodi ya miti Dola Milioni 26, kodi ya zuio Dola Milioni 15.7, tozo ya leseni Dola Milioni 20.8, kodi ya makampuni Dola Bilioni 1.01 na gawio la Serikali kutokana na hisa za asilimia 20 sawa na Dola Milioni 40 kwa mwaka.

Halikadhalika, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited kuzingatia ushirikishwaji wa Watanzania katika utoaji wa huduma mbalimbali migodini kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010, na kuzitaka Wizara ya Madini na taasisi zote zinazohusika kuhakikisha mradi unakuwa shirikishi, endelevu na wenye manufaa makubwa kwa Taifa.

Kwa wananchi wa Namtumbo, Rais Dkt. Samia amesema mradi huu utachochea maendeleo kwa kuboresha huduma za kijamii kama barabara, umeme, maji na shule, sambamba na kuvutia wawekezaji wengine katika mnyororo wa thamani wa urani.

Ameeleza kuwa shughuli na mahitaji yatakayotokana na mradi huu yatazalisha fursa nyingi za kibiashara kwa wakazi wa eneo hilo na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.