Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Kiwanda India chawazawadia wakulima wa Tanzania matrekta 10


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete , Alhamisi, Juni 18, 2015, amepokea matreka makubwa 10 ambayo yametolewa na Kampuni ya New Holland Agriculture ya India kama zawadi kwa mkulima wa Tanzania.

Matreka hayo aina ya TD5.90 yametolewa na Kampuni hiyo baada ya Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete kutembelea kiwanda hicho cha New Holland Agriculture kilichoko katika eneo la Greater Noida, nje kidogo ya Mji wa New Delhi, mji mkuu wa India, ambako Rais Kikwete anafanya ziara rasmi ya siku nne kwa mwaliko wa Rais Pranad Mukherjee.

Kiwanda hicho ambacho huzalisha matrekta ya kisasa kabisa 58,000 kwa mwaka kimekuwa kinafanya biashara na Tanzania tokea mwaka 2011 wakati kilipouza matrekta 700 kwa Shirika la Biashara la Jeshi la Kujenga Taifa la SUMA JKT. Mpaka mwisho wa mwaka huu, imepangwa kuwa shirika hilo la JKT litanunua matrekta mengine 300 kwa ajili ya kuboresha na kuleta mageuzi katika kilimo cha Tanzania.

Mbali na kuuza matrekta hayo, New Holland Agriculture ambacho soko lake kuu ni nchi za Ulaya na Marekani pia kimefundisha mafundi mchundo 26 kutoka JKT na walimu wa walimu watano tokea mwaka jana, 2014.

Pamoja na kwamba trekta la New Holland lilianza  kuzalishwa na Kampuni yake mama ya CNH Industrial mwaka 1895, ilikuwa mwaka 1996 wakati New Holland Agriculture ilipoanzisha kiwanda katika Greater Noida, India. Kiwanda hicho kinamilikiwa kwa asilimia 100 na CNH Industrial.

Kampuni hiyo ya New Holland Agriculture ni moja ya makampuni ambayo yanaongoza dunia kwa kutengeneza vifaa vya kilimo na hasa matrekta ya kulimia na matrekta makubwa ya kuvunia mazao (harvesters).

Kampuni mama ya CNH Industrial ni kampuni kiongozi wa utengenezaji wa vifaa mbali mbali vya viwandani ikiwa inaendesha shughuli zake katika nchi 190 duniani na kutengeneza aina 12 za vifaa katika viwanda 62 na vituo vyake vya utafiti 48, shughuli ambazo kwa pamoja zinaajiri watu 71,000.

Imetolewa na;

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu – Dar es Salaam.

19 Juni, 2015