Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Rais Kikwete atoa Changamoto kwa Sekta Binafsi


SERIKALI imetoa changamoto kwa vyama mbalimbali vya sekta binafsi nchini kuhakikisha kuwa taarifa za fursa za biashara zinawafikia wafanyabiashara ili kutumia vyema fursa zinazojitokeza kwa sasa.

Wito huo umetolewa na Rais Jakaya Kikwete alipokuwa anazungumza wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dar es Salaam juzi.

“Nina imani kuna mengi ya kufaidi kwenu nyote,” alisema, na kuongeza kuwa Serikali iko tayari kufanya kazi na sekta binafsi. Alisema sera ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na ya umma (PPP) ya mwaka 2010 ni kigezo kikubwa kinachoonesha utayari wa serikali kufanya kazi na kuiimarisha sekta binafsi katika kutafuta maendeleo.

“Tunataka sekta binafsi iwe mshirika mkubwa wa maendeleo,” alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa, Serikali imegundua maeneo kadhaa ambayo yanahitaji kurekebishwa katika sera hiyo ya PPP ili kuiimarisha zaidi.

Alisema hivi karibuni serikali itaimarisha kitengo cha PPP katika Ofisi ya Waziri Mkuu ili kusaidia kuimarisha kitengo hicho katika wizara ya Fedha.

Pia alisema serikali itazingatia mchango na maoni yaliyotolewa na wadau wa sekta binafsi kuhusiana na juhudi zinazoendelea za kutengenezwa kwa sera ya taifa ya maendeleo ya sekta binafsi.

Alisema inatambua mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa na kuwa itaendelea kusaidia ukuaji wake. Naye Mwenyekiti wa TPSF aliyemaliza muda wake, Esther Mkwizu aliishukuru serikali kwa uamuzi wa kuhakikisha sekta binafsi inakua na kuimarika nchini.

Alisema sekta binafsi inashukuru kwa nia njema ya serikali kushirikishwa katika mikakati mbalimbali ya hatua za kufikia maendeleo nchini.

Alisema ushiriki wa sekta binafsi katika mkutano wa majadiliano ya ushirikiano wa manufaa kwa wote 2013 ulikuwa wa muhimu na kwamba wataendelea kutoa ushirikiano kwa mijadala kama hiyo katika siku zijazo.