Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Rais Kikwete: Nitaendelea kulikemea suala la udini


RAIS Jakaya Kikwete, ameonya kuwa ushabiki wa baadhi ya viongozi wa dini kuingiza udini katika siasa na kama jambo hilo litakubaliwa kuwa sehemu ya uendeshaji siasa, bila shaka utakuwa mwisho wa utulivu wa Tanzania. Kauli hiyo aliitoa Rais Kikwete mjini hapa hivi karibuni, wakati alipozungumza na viongozi wa Kagera wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku sita mkoani humo.

Aidha, alisema hata kama baadhi ya viongozi wa dini wanamchukia kwa kulisemea jambo hilo hadharani, ataendelea kulisemea bila woga wala kificho, kwa sababu kuitumbukiza dini katika siasa ni kuipeleka nchi mahali kusipo stahili.

Alisema ni jambo la hatari kwa baadhi ya Watanzania ambao ni viongozi kushabikia jambo hilo, kwa sababu mivutano na ugomvi wa kidini sio ajenda ya Tanzania na kwa baadhi ya viongozi wa dini zote kujitumbukiza katika suala hilo ni kucheza ngoma isiyo yetu.

“Wako watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi yetu kwa udi na uvumba na baadhi yetu tumetumbukia katika hilo kwa kupitia udini na siasa. Inashangaza kuona kuna mivutano ya kidini nchini kwa sababu hakuna kitabu kipya cha dini kilichotolewa na dini yoyote hapa nchini. Vita vitakatifu ni vile vile, lakini bado mwelekeo wa dini katika nchi yetu umebadilika na mahubiri ya msingi ni yale yale.

“Ukweli ni kwamba, ajenda ya udini siyo ajenda ya Watanzania, siyo ajenda yetu, hata kama baadhi yetu wanashabikia kupitia siasa ambayo ni hatari kweli kweli. Ndugu zangu nawashaurini tusicheze ngoma isiyo yetu, unyago huu siyo wetu sisi.

“Nichukieni tu lakini nitaendelea kulisemea hili. Wanachukua udini na kuutumbukiza katika siasa na likizama huko halitoki tena. Linalofuata ni kutengeneza siasa za watu wa dini yako, kuchaguliwa kwa dini yako na siyo kwa sifa na uwezo. Jambo hili siku likiingia kweli kwenye siasa huo ndio utakuwa mwisho wa utulivu wa nchi hii.

“Jambo hili halina maana, halina faida wala busara yoyote. Litawagawa wananchi wetu kwa misingi ya dini. Inashangaza kwamba wapo viongozi wa dini zote mbili wanalishabikia hili, jambo litakalofuata ni kutugawa na kuigawa nchi hii, nusu Wakristo, nusu Waislamu,” alisema Rais Kikwete.

Aidha, alipongeza ushirikiano wa viongozi wa dini mkoani Kagera, akisisitiza kuwa uhusiano huo ni muhimu na unafaa kuendelezwa na kuwekewa misingi imara zaidi.